Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Gasto Mkono
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Shinyanga inawashikilia watumishi watatu wa wakala wa barabara mjini na vijijini (TARURA) mkoani hapa kwa tuhuma za kukutwa na fedha za Rushwa walizokuwa wamepewa na wakandarasi kwa ajili ya kuwapitisha kwenye zabuni za ujenzi wa barabara mkoani Shinyanga.
Watumishi hao watatu waliokamatwa kwa tuhuma ya rushwa ni Njama Kinyemi, Rose Mpuya ambao ni maofisa ugavi TARURA mkoa, pamoja na Matoke Chiyando ambaye ni mhandisi TARURA halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Gasto Mkono alisema baada ya kupata taarifa juu ya kuwepo kwa rushwa hizo ndipo wakaanza kulifanyia kazi na hatimaye kufanikiwa kuwakamata watumishi hao wakiwa na fedha za rushwa na kisha kuwasweka rumande kuendelea na uchunguzi zaidi.
“Tumewakata watumishi hao watatu wa TARURA ambao walikuwa kwenye kamati ya kujadili zabuni za ujenzi wa barabara za wilaya zote mkoani Shinyanga, ambapo walikuwa wakiomba rushwa kutoka kwa wakandarasi na baadhi ya fedha wameshawekewa kwenye akaunti zao na zingine zilikuwa kwenye mabegi na mifuko” ,alisema Mkono.
“Watumishi hawa wote watatu tunawashikilia na wapo mbaroni tunaendelea na uchunguzi zaidi na upelelezi ukikamilika tutawafikisha mahakamani ,”aliongeza.
Kwa upande wake mratibu wa Wakala wa barabara TARURA mkoani Shinyanga Ezekiel Kunyarara alisema yupo safarini, hivyo na kuomba waandishi wa habari wawasiliane na Ofisa utumishi Jafari Mwenda ambaye alikiri kukamatwa kwa watumishi hao, na kubainisha sakata hilo hawezi kulizungumzia zaidi mpaka bosi wake huyo.
Na Marco Maduhu- Malunde1 blog
Post A Comment: