Spika wa Bunge Job Ndugai amepiga marufuku wabunge wanawake kuingia bungeni wakiwa wamebandika kucha na kope za bandia.
Spika Ndugai alitoa kauli hiyo jana bungeni muda mfupi baada ya Naibu Waziri wa afya, Dk Faustin Ndugulile kutoa majibu ya madhara makubwa wanayopata wanawake wanaotumia kucha na kope za bandia.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Fatuma Toufiq ambaye alihoji ni wanawake wangapi wameathirika macho kutokana na matumizi ya kope bandia.
"Kwa mamlaka niliyopewa, napiga marufuku wabunge waliobandika kucha za bandia na kope za bandia kwamba ni marufuku na hilo la kujipodoa bado najadiliana na wataalam wangu," amesema Spika.
Naibu Waziri alisema takribani wagonjwa 700 hupokelewa kwa mwaka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa na matatizo ya ngozi yatokanayo na kumeza vidonge vinavyobadili sura pamoja na vipodozi vyenye kemikali na kuwa watu hao wapo kwenye hatari ya kupata magonjwa ya saratani na ya ngozi.
Naibu Waziri alisema kucha na kope za kubandika si vipodozi kwa mujibu wa sheria ya chakula, dawa na vipodozi sura ya 219 inayosimamiwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
"Kwa mujibu wa sheria hiyo, kipodozi ni kitu chochote kinachotumika kwenye mwili au sehemu ya mwili," alisema Dk Ndugulile.
Chanzo- Nipashe
Post A Comment: