Saa zaidi ya 20 tangu kuzama kivuko cha MV Nyerere, idadi ya watu waliokufa imefikia 86, kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella hadi leo saa 4 na dakika 44 asubuhi Septemba 21, 2018 jumla ya maiti 86 zimeopolewa.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cornel Maghembe amesema kuwa sababu ya kuzama kwa kivuko hicho inasadikika kuwa ilibeba watu zaidi ya 400 ambapo kilizidisha uwezo wake ambao ni watu 101.
Maghembe amesema kuwa imezama mita chache kabla ya kuwasili eneo la Ukara ambapo dereva alipunguza mwendo kuashiria amekaribia kutia nanga ndipo abiria wengi walihamia upande wa lango la kutokea wakiwahi kusogea ili washuke ndipo uzito ulizidi na kupinduka.
“Abiria walipoona mwendo umepunguzwa walikimbilia kuwahi mbele ya lango ili kujiandaa kushuka, ndipo uzito ukaegemea upande mmoja”, amesema Maghembe
Baada ya kusitishwa kwa zoezi la uokoaji wa abiria wa ajali ya kivuko cha MV. Nyerere jana jioni baada ya giza kuingia, limeendelea leo alfajiri ambapo hadi sasa waokoaji waliozama majini bado hawajatoka.
Akizungumza na East Africa Radio, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi Jonathan Shana, amesema kuwa tayari kikosi cha uokoaji kimeshaanza uokoaji tangu saa 11 alfajiri ambapo hadi walipositisha zoezi hilo tayari walikuwa wameopoa miili 44 na waliohai 32.
Chanzo-EATV
Post A Comment: