Waziri  wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Selemani Jafo, ametoa miezi miwili kwa Wakala wa Majengo (TBA) kukamilisha ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni zinazojengwa katika eneo la Gezaulole.

Ujenzi wa ofisi hizo ulianza Januari mwaka huu na ulitakiwa kukamilika Agosti lakini hadi sasa haujakamilika na TBA wameomba kuongezewa muda hadi Januari mwakani.

Akizungumza jana baada ya kukagua ujenzi huo, alisema ofisi zinazotumika sasa ni finyu na kumtaka mkandarasi huyo kukamilisha angalau gorofa moja ifikapo mwishoni mwa Novemba ili ofisi zihamishwe.

“Haiwezekani watu waendelee kukaa kwenye ofisi ambayo iko kama ‘briefcase’ hata sehemu ya kusaini ni shida, naagiza mwishoni mwa mwezi wa 11 iwe jua iwe mvua mkurugenzi na watumishi wako muwe mmehamia hapa,” alisema Jafo.

Naye Mwakilishi wa TBA, Edwin Godfrey, alisema wameshindwa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati kwa sababu wakati wanaanza msingi walikumbana na changamoto ya mvua.

Gharama ya ujenzi huo ni Sh bilioni 5.1 na hadi sasa TBA wameshapokea Sh bilioni 1.35.

Katika hatua nyingine Waziri huyo aliipongeza manispaa hiyo kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Kimbiji lakini akawapa muda hadi ifikapo Novemba 30 mwaka huu wawe wamekamilisha ujenzi wa jengo katika Kituo cha Afya Kigamboni.

Kwa mujibu wa Jafo, manispaa hiyo ilipewa fedha za ujenzi huo Juni 26 mwaka huu na kuagizwa hadi kufikia Oktoba 30 majengo yawe yamekamilika lakini hadi sasa ujenzi haujaanza.

“Wakurugenzi wapya nendeni kwa kasi kubwa, nataka muwe mfano katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.

“DED (Mkurugenzi wa Halmashauri) Kakonko amejenga jengo zuri na tayari limekamilika kwa Sh milioni 700. Pangani walipewa Sh bilioni 1.5 lakini hata hawajui lini jengo lao litaisha,” alisema Jafo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema wana changamoto kubwa ya usimamizi na kumuomba waziri huyo kubadilisha mfumo wa wakuu wa idara ili wawe wanapimwa kwa matokeo na si uzoefu wa kazi.

“Tumeshamwandikia Waziri wa Utumishi ili wakuu wa idara waanze kuwajibika kulingana na matokeo, wakurugenzi waanze kuwapima wakuu wao wa idara,” alisema Makonda.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: