Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba akifungua mkutano wa wadau wa Mazingira Jijini Arusha. Mkutano huo umeshirikisha wadau mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali na zile zisizo za kiserikali kwa lengo la kujadili changamoto ya mimea vamizi yenye athari hapa nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba akifuatilia mawasilisho ya mimea vamizi kutoka kwa Mtaalamu wa COSTECH (hayupo pichani). Kulia ni Mhe. Nape Nnauye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi na Maliasili.
Sehemu ya Washiriki wa Mkutano wa wadau wa kujadili changamoto za mimea vamizi. Mkutano umefanyika katika ukumbi wa AICC jijini Arusha. Mstari wa mbele katika picha ni waheshimiwa wabunge waliohudhuria.
KATIKA jitahada za kupambana na mimea vamizi nchini ambayo kwa kiasi kikubwa ina athari kwa uchumi wa Nchi yetu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba hii leo amewakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali, asasi za kiserikali na zisizo za kiserikali, Wenyeviti wa Kamati za Bunge za Ardhi na Maliasili, Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji ili kwa pamoja waweza kujadili namna bora ya kupambana na mimea vamizi ambayo imetapakaa kwa kasi katika maeneo mbalimbali hapa nchi.
“Pamoja na kwamba viumbe vamizi wageni ni janga kwa makazi asilia ya viumbe, lakini hatujalishughulikia kikamilifu, kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kukabiliana na viumbe hivi. Kwa muktadha huo, leo tumepata fursa adimu na adhimu kutafakari kuhusu hali ilivyo kwa sasa, changamoto zilizopo na kujadili mikakati madhubuti ya kukabiliana na tatizo la viumbe vamizi wageni hapa nchini” Makamba alisisitiza.
Wadau waliohudhuria mkutano huo wameitaka Serikali kuongeza nguvu katika kupambana na tatizo hilo kwa kuibua miradi mbalimbali kote nchini ili kwa pamoja kuwa na mkakati wa kitaifa wa kupambana na hali hiyo ambayo ina athari kubwa kiutalii.
Mhe. Innocent Bashungwa Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira amesema kuwa suala kubwa ni kuuongeza bajeti kila mwaka katika sekta ya usimamizi wa mazingira pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa Mazingira.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Murad Sadick amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais iunde kikosi kazi cha kusimamia jambo husika na kulipa kipaumbele kama hatua za haraka, ikiwa ni pamoja na kuitaka Serikali kutenga fedha nyingi katika suala la utafiti ambao utasaidia kuja na suluhu katika changamoto hiyo.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Mahmoud Mgimwa amesema kuwa kwa uwakilishi wao wa Kamati hizo tatu, jumla ya wabunge 75 kutoka Kamati wanazo ziongoza wameshafahamu tatizo hilo. “Sisi tuko tayari kuunga mkono upatikanaji wa fedha ili kuendesha tafiti mbalimbali, kama hatua za dharura na kuhakikisha Sheria iliyounda Mamlaka ya Ngorongoro inapitiwa upya ikiwa ni pamoja na kutokujenga majengo ya kudumu ili kutoathiri ikolojia ya eneo hilo.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili na Utalii Mhe. Nape Nnauye amesema Kamati yake ya Maliasili na Utalii na Bunge kwa ujumla watachukua hatua kama janga la Kitaifa, “Tunazungumzia uhai wetu sisi, athari za mimea na wanyama zinaathiri binadamu, hivyo lazima tupambane kwa nguvu zote kutokomeza hili jambo, madhara yake ni makubwa kwetu sisi binadamu”.
Mhe. Nnauye amewataka watafiti kutumia uzoefu kutoka nchi nyingine kuleta uhalisia katika nchi yetu na kuondoa dhana potofu ya kuamini kuwa kila tatizo jibu lake ni siasa. “Nyinyi wasomi, wataalamu andaeni majibu ya matatizo, nashauri kiundwe kikosi kazi na kuandaa majibu kwa makundi, sera, sheria, kanuni, bajeti, hamasa na usimamizi” Mhe. Nape alifafanua.
Waziri Makamba amesema kuwa pamoja na kwamba zipo Sera na Sheria mbalimbali zinazo simamia udhibiti wa viumbe vamizi wageni nchini ikiwemo sekta za Kilimo, Misitu, Uvuvi, Wanyamapori, Mifugo na Mazingira na Kanuni za Udhibiti wa Magugu Maji (2001), lakini suala hili halijapata utatuzi mahiri, hivyo msukumo zaidi na ushirikiano wa pamoja wa sekta zote katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hii unahitajika.
Mhe. Makamba amesema kuwa yeye kama Waziri mwenye dhamana ya Mazingira anayo mamlaka kupitia sheria ya mazingira kifungu cha 66 3 (a) “Waziri kwa kushauriana na Wizara ya sekta husika anaweza kutunga kanuni zinazo agiza kutengeneza mikakati. Programu na mipango ya kitaifa ya hifadhi na matumizi endelevu ya bioanuai”. Aidha, kifungu cha 67 2 (f) “Waziri kwa kushauriana na Wizara ya sekta anaweza kuandaa kanuni zinazoweza kubainisha ukarabati na urejeshaji mifumo ikolojia iliyoharibiwa na kuendeleza urejeshwaji wa sipishi zilizoko hatarini, pamoja na mengineyo, kwa kuendeleza na kutekeleza mipango, mikakati mingine ya usimamizi” .
Mwenyekiti wa Kikao hicho Waziri Makamba amesema mkutano huo ni mwanzo wa suluhisho la kudumu la kupata majawabu katika kuratibu utokomezaji wa mimea vamizi. “Nitaunda kikosi kazi cha kitaifa ndani ya wiki moja ijayo ili kiweze kushughulikia jambo hili na kuleta mapendekezo yatakayoleta andiko la kuchukua kama hatua za haraka, kwa mwezi mmoja” Makamba alisisitiza.
Changamoto ya viumbe vamizi wageni inagusa sekta muhimu kwa uchumi wetu ikiwemo kilimo, misitu, uvuvi, mifugo, wanyamapori, utalii na hata shughuli za uchukuzi majini.
Post A Comment: