Picha hii haihusiani na tukio.
Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari ya Kambangwa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambaye alipatwa na uchungu wa kujifungua akiwa darasani amesema, mpaka anakaribia kujifungua si yeye wazazi wala walimu waliojua kuwa ni mjamzito.
“Nilivyopatwa na ujauzito, hakuna mtu aliyejua ila kuna watu wakawa wananiambia Maria mbona unanenepa sana na unatembea kama unainama. Walimu wakaniita na kuniuliza nina tatizo gani, nikawambia mimi sina tatizo, wakaniambia nina ujauzito. Wakamuita baba na kumueleza, kesho yake niliporudi shule tumbo likaanza kuniuma, nikakimbizwa hospitali nikajifungua.” amesema mwanafunzi huyo.
Mwanafunzi huyo ambaye kwa sasa amefukuzwa masomo, amesema ndoto yake kubwa ilikuwa kuja kuwa daktari, lakini ujauzito aliupata kwa kurubuniwa na kijana mmoja (jina limehifadhiwa kwa sasa) , ambaye ni mkazi wa Kinondoni Mahakamani, amekatisha ndoto zake ingawa yupo tayari kurudi masomoni na kuipigania ndoto yake au kwenda chuo cha ufundi.
Kupitia East Africa Breakfast ameomba watanzania na asasi za kiraia zimsaidie aweze kutimiza ndoto yake ya kusoma na hatimaye aweze kujitegemea kwani familia yake ni masikini. Anasema anajutia kosa alilolifanya kutokana na kurubuniwa na kupata ujauzito, lakini anaamini bado anayo nafasi ya kujisahihisha.
Mama mzazi wa mtoto huyo ameieleza East Africa Breakfast ya East Africa Radio, kuwa mtoto wake alikuwa akipata mabadiliko makubwa ya mwili lakini yeye alihisi ni kawaida mpaka pale alipotakiwa na walimu kumchunguza vizuri mtoto huyo, lakini siku moja tu baada ya kubaini ukweli wa suala hilo, alishtuka kuambiwa mtoto wake ameshikwa na uchungu akiwa darasani na kutakiwa kumuwahisha hospitali ambapo alienda kujifungua.
Chanzo-EATV
Post A Comment: