Joyce Ngalama (27), mtumishi Hospitali ya Wilaya Igunga mkoa wa Tabora kitengo cha takwimu anashikiliwa na polisi kwa mahojiano akituhumiwa kumuunguza kwa pasi mfanyakazi wake wa ndani mwenye umri wa miaka 13.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni utekelezaji wa amri ya mkuu wa wilaya ya Igunga, John Mwaipopo baada ya kupokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa raia wema.
Akizungumza leo Septemba 7, 2018 Mwaipopo amesema raia wema waliompa taarifa wamemjulisha kuwa binti huyo aliyechukuliwa na mtuhumiwa akitokea nyumbani kwao mkoani Kigoma, amekuwa akiadhibiwa kwa vipigo vya mara kwa mara.
“Baada ya kupokea taarifa hizo, nilimwagiza OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) wa Igunga kumtia mbaroni mtuhumiwa,” amesema.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo ana majeraha sehemu mbalimbali za mwili zinazodaiwa ni kutokana na kipigo. Uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.”
Wakizungumzia tukio hilo kwa nyakati tofauti, baadhi ya majirani Ashura Ramadhani, Flora Jackson na Rachel Samson wamesema walisikia kelele za kilio cha mtoto huyo na walipokwenda kujua tatizo, mtuhumiwa aliwaeleza kuwa amemwadhibu kwa kosa la kutoosha chupa ya uji wa mtoto na tabia ya kukojoa kitandani.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Masanga anakoishi mtuhumiwa, Julias Kitundu amewataka wazazi na walezi kuacha kuwafanyia watoto wao au wale wanaoishi nao vitendo vya ukatili huku akionya kuwa ofisi yake haitafumbia macho vitendo hivyo.
Na Robert Kakwesi, Mwananchi
Post A Comment: