Maafisa wa polisi wamewakamata watu sita kuhusiana na ubakaji wa kikundi na mauaji ya msichana wa miaka tisa nchini India katika jimbo la Kashmir.
Maafisa wanasema kuwa mama wa kambo wa msichana huyo alimwambia mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka 14 na wengine watatu kumbaka msichana huyo mbele yake.
Wanasema kuwa mwili wa msichana huyo ulipatikana siku ya Jumapili katika msitu wilayani Baramulla.
Aliteswa na mwili wake kuchomwa na tindi kali , waliongezea.
Mama huyo wa kambo anadaiwa kukasirishwa kwa kuwa msichana huyo alikuwa akipendwa sana na mumewe.
Maafisa wa polisi waliambia BBC Urdu kwamba msichana huyo alitoweka kwa siku kumi kabla ya mwili wake kupatikana.
Ilibainika kwamba mama huyo wa kambo alikuwa na chuki dhidi ya mke wa pili wa mumewe na watoto wake , mtandao wa kituo cha habari cha NDTV kilimnukuu afisa mmoja wa polisi Miir Imtiyaz Hussain akisema.
Bwana Hussein alisema kuwa msichana huyo aliuawa kwa shoka baada ya kubakwa na genge.
Alisema kuwa mmoja ya washukiwa mwenye umri wa miaka 19 alimpiga na kumjeruhi vibaya mwilini.
Hii ni mara ya pili ubakaji mbaya wa aina hiyo umefanyika katika jimbo la Kashmir katika miezi ya hivi karibuni.
Mnamo mwezi Aprili, msichana Muislamu wa miaka minane kutoka Wilaya ya Kathua alibakwa na genge na kuuwawa.
Hatua hiyo ilizua hisia kali baada ya mawaziri wawili kutoka chama cha Hindu Bharatiya BJP kuhudhuria mkutano kuwaunga mkono washukiwa ambao ni Wahindu.
Tatizo la unyanyasji wa kingono nchini India limeongezeka tangu ubakaji wa genge mwaka 2012 na mauaji ya mwanafunzi wa miaka 23 katika basi katika mji mkuu wa Delhi.
Uhalifu huo ulisababisha maandamano ya siku kadhaa na kuilazimu serikali kubuni sheria kali dhidi ya ubakaji ikiwemo hukumu ya kifo.
Hata hivyo mashambulio dhidi ya wanawake na watoto yanaendelea kuripotiwa nchini humo.
Chanzo - BBC
Post A Comment: