Na Felix Mwagara, MOHA-Kibondo
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametoa wiki mbili kwa Jeshi Polisi Mkoa wa Kigoma, kuhakikisha linakomesha matukio ya ujambazi yaliyokithiri katika Wilaya ya Kibondo pamoja na sehemu zingine mkoani humo.

Lugola aliongeza kua, katika kupambana na majambazi hao ambao wanasumbua wananchi  wilaya hiyo ya Kibondo na kukosa amani katika maeneo yao, polisi ifanye operesheni maalumu kuwatia mbaroni watuhumiwa hao.  

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Community Centre mjini Kibondo, leo, Lugola alisema katika operesheni hiyo pia itambatana na utoaji onyo kwa watu wasio waaminifu wanaowahifadhi raia wa kigeni ambao wengi wao ni wahalifu.

‘’Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, natoa wiki mbili tu, kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya fanyeni operesheni ya kuwasaka majambazi hawa usiku na mchana mpaka jambazi wa mwisho awe amekamatwa,’’ alisema Lugola.

Lugola alisema haiwezekani tukasalimu amri kwa majambazi, haiwezekani kunyoosha mikono kwa jambazi  waliopo katika maeneo mbalimbali wa wilaya hiyo pamoja na mkoa kwa ujumla.

Waziri Lugola pia aliwataka wananchi wilayani humo kutoa taarifa polisi za wahalifu hao ili kuwezesha operesheni hiyo ifanikiwe zaidi na wananchi waweze kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao za kuijenga nchi.

Waziri huyo pia licha ya kusema anajua changamoto mbalimbali zinazowakibili polisi ikwemo ukosefu wa magari lakini aliwataka aliwataka wawahi katika  matukio ya uhalifu yanapotokea, wanaweza kutumia pikipiki ili kuwahi kwa wakati katika matukio hayo.

Waziri Lugola yupo katika ziara ya kikazi Mkoa wa Kigoma ambapo anatembelea Wilaya zote mkoani humo kwa kufanya kikao na watumishi walio chini ya wizara yake pamoja na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwa ajili ya kusikiliza kero zao pamoja na kuzitatua.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: