Baada ya kutangazwa kama mshindi wa uchaguzi mdogo wa marudio katika jimbo la Ukonga kupitia chama cha Mapinduzi CCM, Mwita Waitara, amesema mawakala wa CHADEMA katika vituo vya kupigia kura walimpigia yeye.
Akiongea leo baada ya kutangazwa, Mwita amesema alikuwa na matarajio ya kushinda kwa zaidi ya asilimia 95, hivyo hajashangaa kupata ushindi huo wa asilimia 89.
''Nina ushahidi wa ujumbe mfupi kwenye simu yangu, mawakala wa CHADEMA katika vituo jana wamenipigia kura na walikuwa wananitumia matokeo mapema tu hiyo inaonesha nilikuwa na uungwaji mkono mkubwa sana'', amesema.
Aidha Mwita amekishauri chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kujitazama kilipojikwaa na sio kilipo angukia huku akiweka wazi kuwa kama wanataka chama kibakie waachane na mwenyekiti wao Freeman Mbowe na wakiendelea kumkumbatia chama kitawafia.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi leo, msimamizi mkuu wa uchaguzi jimbo hilo, Jumanne Mashauri amemtaja Mwita Waitara wa CCM kama mshindi wa kiti cha ubunge baada ya kupata kura 77,795 sawa na asilimia 89.1 huku mpinzani wake, Asia Daudi Msangi ( CHADEMA) akipata kura 8,676 sawa na asilimia 9.95
Post A Comment: