Polisi mkoani Mwanza wanamshikilia binti wa miaka 20, Sonia Fanuel mkazi wa Nyegezi, Mwanza kwa tuhuma za kukutwa na funguo bandia 154.

Kati ya funguo hizo, 53 zinadaiwa kuwa ni za vitasa na 101 ni za kufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna alisema msichana huyo alikamatwa juzi saa 1:45 usiku katika Mtaa wa Rose, Nyegezi ambako anadaiwa kuwa alikuwa akifanya uhalifu.

Kamanda Shanna alisema, Sonia alikamatwa baada ya wasichana wawili, Esther Isaack na Ruth Sumali, wakazi wa Mtaa wa Rose, Nyegezi, kukuta milango ya vyumba vyao imefunguliwa huku Sonia akiwa amejibanza ukutani.

Alisema walipokagua mali zao ndani, walibaini Sh160,000 zimeibwa na nguo zenye thamani ya Sh200,000. Kamanda huyo alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani upelelezi ukikamilika.

Awalevya wanawake, awabaka

Katika tukio jingine, mkazi wa Mwanza, Kenned Obworo (35), amekamatwa na polisi akituhumiwa kuwanywesha dawa za kulevya wanawake na kisha kuwabaka na kuwaibia.

Shanna alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Jumanne iliyopita katika Hoteli ya Jawita, Mtaa wa Rufiji saa mbili asubuhi na kwamba katika uchunguzi, polisi wamebaini kuwa amekuwa akiwalaghai wanawake kwa kuwanunulia chakula na vinywaji kisha kuwawekea dawa zinazodhaniwa kuwa ni za kulevya ili awabake, kuwaibia fedha na simu za mkononi, kazi ambayo anadaiwa kuifanya kwenye nyumba za wageni ambazo anakuwa amekodisha.

Kamanda Shana alisema Jumatano iliyopita, saa mbili usiku katika Hoteli ya Haven iliyopo Nyasaka, Ilemela alimchukua mwanamke mmoja na kumnunulia Red Bull kisha akamuwekea dawa hizo na baada ya kulewa alimuingiza chumbani na kumbaka.

Alisema tukio kama hilo lilitokea Magu Jumatatu iliyopita katika baa iitwayo Dear Sija Lodge.

Alisema kabla ya tukio hilo, wanawake wanne walikutana na mtuhumiwa huyo katika baa ya Villa Park, Mwanza ambao walimuomba awanunulie vinywaji. Alifanya hivyo kisha wakapeana namba za simu na kuachana salama.

Alisema wanawake wawili kati ya wanne, walimpigia simu wakakubaliana wakutane tena Villa Park na walipokutana waliafikiana waende Kisesa kwa kutumia gari la mmoja wa wanawake hao.

Baada ya kufika Dear Sija, Kamanda Shanna alisema waliagiza vinywaji kisha wanaume wawili akiwamo mtuhumiwa waliingia chumbani na kuwaingiza wanawake hao ambao waliwalevya na kuwabaka kisha kuwaibia simu mbili za Sumsung na kuwaacha hawajitambui.

Alisema baada ya kufanya upekuzi kwenye vyumba hivyo walikuta vidonge aina ya Lorenzepam na mtuhumiwa amekiri kufanya matukio kama hayo katika mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Mara, Arusha na Mwanza.

Alisema uchunguzi wa awali unaonyesh kuwa vidonge hivyo aina ya Lorivan 2 na Lorenzepam ni dawa zinazotumiwa kwa wagonjwa wa akili ili kuwapa usingizi au kuwalevya wakati wa kupatiwa matibabu.
Na Jesse Mikofu na Johari Shani mwananchi
Share To:

Anonymous

Post A Comment: