Na Tumaini Msowoya, Mwananchi 

Wakati mwili wa mwimbaji wa kwaya ya Vijana ya Kanisa la AICT, Chang’ombe jijini Dar es Salaam, Mariam Charles ukizikwa kwenye makaburi ya Maduka Mawili-Chang’ombe jana, mtu anayedaiwa kumuua amekamatwa na polisi kwenye nyumba ya wageni iliyo jirani na kanisa hilo maeneo ya Sokota.

Akielezea namna mtuhumiwa huyo alivyokamatwa, meneja wa nyumba ya kulala wageni ya Kisuma iliyopo maeneo ya Sokota-Chang’ombe, Damian Urio alisema mtuhumiwa ambaye alijiandikisha kwa jina la Frank Magulu alifika katika nyumba hiyo ya wageni ambayo inapakana na kanisa la AICT juzi jioni.

Urio alisema baada ya mteja huyo kufika katika ‘gesti’ hiyo, mhudumu alimpangisha chumba namba 230 alimolala hadi jana asubuhi.

“Alikuja jana (juzi) japo majira sikumbuki vizuri, lakini alifika akapewa chumba. Aliingia na baadaye akatoka kidogo, hakukaa sana akarudi kulala,” alisema Urio.

Alisema kwa kuwa hawakujua chochote walimhudumia kama wateja wengine.

“Leo hii (jana) saa tano mhudumu alimgongea chumbani akamwambia atoke afanye usafi. Lakini mteja aliomba maji ya kopo akaambiwa mbona bafuni yapo? akasema anataka hayo, basi akapewa na kunawa.”

Alisema baada ya kunawa alitoka kwenda kutafuta chai na aliporudi akaingia tena chumbani, lakini alionekana kama amechanganyikiwa kwa kuwa alikuwa hatulii. “Basi alitoka chumbani akaja mapokezi wakati anaongea ghafla tukashangaa polisi wameingia na kumkamata,” alisema Urio.

“Kwenye kitabu jana aliandika jina lake kamili la Frank Magulu analotumia, lakini alikuwa kama hana raha.”

Wakati mtuhumiwa huyo akikamatwa na polisi gesti, upande wa pili kama mwendo wa dakika moja lilipo kanisa la AICT, ibada ya kumuaga Mariam ilikuwa ikiendelea.


Polisi waelezea

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula amesema jana walifanikiwa kumtia mtuhumiwa mbaroni wakati akijiandaa kuingia nyumba ya kulala wageni ya Kisuma iliyoko maeneo ya Sokota.

Alisema kuwa walimpeleka hospitali ya Temeke baada ya kuwaambia kuwa amekunywa vidonge kumi vya valium na konyagi ili afe kama Mariam.

“Mtuhumiwa anafahamika kwa majina ya Nandi Joseph Magulu au Frank Joseph Magulu, miaka 29,” alisema.

Kamanda Lukula alisema mtuhumiwa huyo ni mtaalamu wa maabara na ni mkazi wa Kilakala, Temeke.

“Mtuhumiwa amekutwa na daftari aliloandika kujutia kumuua marehemu kwa wivu wa mapenzi,” alisema kamanda.

Shuhuda azungumza

Mmoja wa watu walioshuhudia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo alisema huenda baada ya msiba angesababisha tukio jingine kama alivyokuwa anasambaza ujumbe.

Shuhuda huyo ambaye ni mmoja wa wanakwaya hao wanaotamba na albamu ya Pazia la Hekalu, alisema mtuhumiwa alijiunga nao mwaka mmoja uliopita.

Alisema wakati anajiunga na kwaya hiyo alikuwa akitokea mkoani Shinyanga.

“Alijiunga na kwaya na kwa sababu hapa kwetu kuna utaratibu wa kuhakikisha walau kijana awe na kazi alisaidiwa na kupata kazi ya maabara kwa sababu ni fani yake,” alisema mwanakwaya huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Alisema wakati akiendelea na kazi alidaiwa kumuibiwa mwajiri wake na kuamua kukimbia. “Kwa hiyo aliporudi ndiyo sasa tukio hili likatokea, alikuwa kwenye mahusiano halali ya uchumba na ukimuona hakuwa anaonyesha kama anaweza kufanya unyama huo,” alisema.

Mwili wa Mariam (26), ulikutwa kwenye nyumba ya wageni ya East London iliyopo Buza anakodaiwa alikuwa na mchumba wake usiku wa kuamkia Jumatano.

Viongozi wa kanisa

Akihubiri jana katika ibada kanisani hapo wakati wa kumuaga Mariam, mchungaji kiongozi wa kanisa hilo, Elisha Isebuka alisema ilikuwa vigumu kupokea msiba huo na kwamba hakuamini alipoelezwa na wazazi wa marehemu.

“Tunatambua Mariam alikuwa sehemu yetu na leo hayupo. Hata hivyo tunamshukuru Mungu hata katika hili najua tunapitishwa kwenye wakati mgumu ambao tunaweza kulaumu, lakini katika yote Mungu atabaki kuwa Mungu,” alisisitiza.

Katibu wa kwaya aliyokuwa akiimba Mariam, Dickson Seni alisema wanapitia katika huzuni kubwa ya kuondokewa na mwenzao lakini hawana budi kumshukuru Mungu kwa jaribu hilo.

“Tutaendelea kumuenzi mwenzetu tukiwa pamoja na wazazi wake, tumehuzunika sana lakini tunaamini hata katika hili bado Mungu hatatuacha,” alisema Seni.

Askofu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Pwani, Charles Salala alisema nyakati yanapotokea matukio ya kutisha kama hilo ni wakati wa kumtafakari Mungu.

“Hili tuliache mikononi mwa Mungu mwenyewe na niwape pole wazazi, ndugu, wanakwaya wenzake na waumini wote,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo juzi, mama mzazi wa Mariam, Esther Lutonja alisema binti yake alimuaga kwenda kuonana na mchumba wake mchana wa Jumanne na hakurudi. Baadaye, Ester alisema Jumatano alitumiwa ujumbe mfupi wa simu na mchumba wa mwanaye uliosema, “tayari nimemuua mwanao”.

Hata baada ya mwili wa Mariam kupatikana, mtuhumiwa alidaiwa kuendelea kutuma ujumbe wa vitisho kwa ndugu wa marehemu. 

Ndugu hao walisema kuna wakati mtuhumiwa alitumia simu yake na wakati mwingine simu ya Mariam.

Akizungumzia ujumbe huo, dada wa Mariam, Lucy Enock alisema baadhi ya wanafamilia wametumiwa ujumbe wa vitisho kwa simu aliyokuwa anatumia mdogo wake.

Alisema ametumiwa ujumbe kwa namba ya Mariam unaosema: 

“Nimemuua Mariam kwa ajili ya uongo wake kwangu na alinitengenezea njama kwa mama Kashimba ili nikamatwe, nikamgundua baada ya mama huyo kumpigia akiwa anaoga...”

Ndugu mwingine wa marehemu, Paul Makelele alisema amepokea vitisho kutoka kwenye namba ya Mariam.

“Kuna meseji nimetumiwa, inasema: “Mtindo wako wa kushindwa kutunza siri nina silaha au nikufuate? Ni meseji nyingi napokea,” alisema.

Meseji nyingine aliyotumiwa ilisema:

“Jamani kama kukimbia ningeweza, maana nilikuwa nimefika nje ya mji, saa hivi nimerudi naenda polisi mwenyewe, hata kujiua nashindwa hata nikijaribu kwa sababu sijaua kwa kukusudia,”

Ujumbe huo mfupi uliendelea kusema: “Ni bora kuuliwa kuliko mateso ya nafsi ya Mariam ninayoyapata. Mariam ananitokea kila nikitaka kujiua...”

Mauaji ya wenza

Akizungumzia tukio la aina hiyo, daktari wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Omari Ubuguyu alisema kisaikolojia kuna mambo mengi yanayomfanya mtu aue.

Alisema mbali ya mambo hayo, yapo mengine makuu matatu ambayo ni magonjwa ya akili, tatizo la kisaikolojia na ya kijamii ikiwamo yanayoaminiwa na watu.

Dk Ubuguyu alifafanua kuwa katika magonjwa ya akili mtu anaweza kuwadhuru watu baada ya kupata hisia za kiugonjwa.

Alisema mtuhusika anaweza kudhani kuwa watu ni wabaya na wanapanga au wanaweza kumdhuru yeye, watu wa karibu au watu wengine.

“Kitaalamu hali hii huwa tunasema wanarespond to psychotic experiences,” alisema. “Watu wenye ugonjwa unaoitwa schizophrenia, delusional disorder (paranoid type) na baadhi ya wagonjwa wa kifafa ni miongoni mwa watu wanaoonyesha kupatwa na shida hii,” alisema Dk Ubuguyu. Mtaalamu wa saikolojia kutoka Muhimbili, Dk Isack Lema alisema licha ya kuwapo kwa mambo mbalimbali yanayosababisha hakuna la moja kwa moja linalohusishwa.

Alisema mtu hufanya hivyo kulingana na kinachomsukuma kwa wakati huo.

“Kwa kawaida anayefanya mauaji kwa hisia huwa ana tatizo la kiafya,” alisema Dk Lema.

“Sasa inaweza kuwa ya mwili, kisaikolojia kutokana na mazingira aliyokulia kwa sababu hakuna binadamu anazaliwa na dhamira ya kuua labda kama ameishi katika mazingira hatarishi kama ya vita, hivyo amekata tamaa.”


Chanzo- Mwananchi
Share To:

Anonymous

Post A Comment: