Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 23, anaripotiwa kufariki dunia, baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuongeza makalio kwa lugha ya kitaalamu Brazilian Butt Lift.


Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, mwanamke huyo, Leah Cambridge kutoka mjini Leeds nchini England, alikutwa na umauti huo, baada ya kusafiri hadi nchini Uturuki kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji huo, lakini wakati kazi hiyo ikiendelea alipata mishtuko mitatu ya moyo.

Mwenzake ambaye aliongozana naye, Scott Franks, aliliambia gazeti la The Sun kwamba mwanamke huyo akifariki baada ya kudungwa sindano ya ganzi katika kliniki moja iliyopo katika mji wa Izmir uliopo Magharibi mwa nchi hii.

“Mrembo huyo alikubali kufanya upasuaji ughaibuni ambapo ni bei nafuu ikilinganishwa na Uingereza baada ya kukerwa na mafuta mengi katika sehemu yake ya tumbo baada ya kupata watoto,” alisema Frank.

Wakizungumza na gazeti hilo, majirani zake walimtaja mwanamke huyo kuwa alikuwa anayevutia na wakasema kwamba wanaamini alienda kufanyiwa upasuaji huo mwezi uliopita bila kumshauri mpenzi wake.

Hata hivyo, Cambridge si mwanamke wa kwanza kutoka Uingereza ambaye amewahi kuwa na hamu ya kuwa na makalio ya kuvutia kupoteza maisha akiwa ughaibuni.

Mwanamke mwingine ambaye aliwahi kukutana na kifo ni Joy Williams ambaye alifanyiwa upasuaji kama huo, Oktoba 2014 mjini Bangkok nchini Thailand, lakini vidonda vyake vilipata maambukizi na mwanamke huyo ambaye alikuwa na umri wa miaka 24, alifariki wakati akidungwa sindano ya ganzi.


Miaka mitatu kabla ya kutokea kifo hicho, Claudia Aderotimi, mwenye umri wa miaka 20 kutoka katika mji wa Hackney, uliopo Mashariki mwa Jiji la London alifariki akiwa hotelini nchini Marekani wakati akipatiwa matibabu ya vidonda vya kujiongeza makalio yake.


Mmoja wa madaktari ambao wanafanya kazi hiyo ya upasuaji, Bryan Mayou, alisema licha ya upasuaji huo wa kuongeza makalio kutoonekana kuwa hatari, lakini ni tishio kama aina nyingine zozote za upasuaji.


“Hatari hiyo inatokana na kuwa upasuaji huo kufanywa na madaktari ambao hawajahitimu, nje ya hospitali bila kuwa na maelezo ya jinsi ya kujichunga baada ya matibabu hayo kufanywa,” alisema Daktari Mayou, ambaye ni mwanachama wa muungano wa madaktari wa upasuaji nchini Uingereza.
Share To:

Anonymous

Post A Comment: