Na Mathias Canal, WK-Simiyu
Waziri
wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba, jana 3 Agosti 2018 amezindua
maadhimisho ya 25 ya Nanenane kwa mwaka 2018 katika Viwanja vya
Nyakabindi, Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu huku akitoa
wito kwa wananchi wote wa mikoa inayounda kanda ya Ziwa Mashariki
ambayo inayojumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga kutumia fursa ya
kutembelea katika maonesho hayo ili kujifunza mbinu mbalimbali za
kitaalamu katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi wa maonesho hayo Dkt Tizeba aliwasihi wananchi wote kutumia fursa ya maonesho hayo kwa kuwatumia ipasavyo wataalamu ambao watakuwepo katika viwanja hivyo kwa siku zote za maonesho hayo ili kupata ushauri na maelekezo ya kuboresha shughuli zao za kiuchumi kupitia Kilimo, Ufugaji, Uvuvi na Ushirika.
Alisema
kuwa wananchi wanapaswa kutembelea katika maonesho hayo kwa lengo la
kujifunza ili kuwa tayari kuanza kutumia teknolojia na maarifa
watakayopata kwa lengo la kujiletea mapinduzi halisi katika kilimo,
mifugo na uvuvi.
Mhe
waziri Tizeba alisema kuwa sekta ya kilimo nchini itaendelea kuwa sekta
muhimu katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla
hususani katika wakati huu ambapo serikali imejidhatiti kufikia uchumi
wa viwanda. Alisema sekta ya kilimo imeendelea kuimarika kwa kuchangia
Pato la Taifa hadi asilimia 30.1 kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na
asilimia 29.2 mwaka 2016.
Sambamba
na hayo Mhe Tizeba alisema kuwa ushirika ni sekta mtambuka inayohusisha
sekta mbalimbali zikiwemo Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Madini, Viwand,
Nyumba na Fedha (Ushirika wa Akiba, Mikopo na Benki) ambazo zinagusa
wananchi wengi zaidi.
Alisema
kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, Wizara kupitia Tume ya maendeleo ya
ushirika imeendelea kuwezesha na kuimarisha ushirika ili wananchi waweze
kunufaika na fursa zinazopatikana katika ushirika kwa lengo la
kuchangia katika kuongeza kipato kwa wananchi wengi hususani waliopo
vijijini.
Alisema
katika mwaka 2017/2018, Tume imefanya uhamasishaji wa wananchi kujiunga
au kuanzisha vyama vya ushirika ambapo hadi kufikia Disemba 2017 vyama
vipya 394 vilisajiliwa na kufanya idadi ya vyama vya ushirika kufikia
10,990 kutoka 10,596 vilivyokuwepo Machi 2017.
Alisema
vyama hivyo vinakadiriwa kutoa ajira mpya kwa wananchi takribani 1,182
huku katika kipindi cha mwaka 2017/2018 wanachama wapya 385,295
walijiunga au kuanzisha vyama vya ushirika na kufanya idadi ya wanachama
kuongezeka kutoka 2,234,016 hadi kufikia 2,619,311
Kilele
cha maadhimisho ya 25 ya Nanenane kwa mwaka 2018 katika Viwanja vya
Nyakabindi, Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu ni Tarehe 8
Agosti 2018 ambapo Rais Mstaafu wa awamu ya tatu nchini Tanzania Mhe
Benjamin Willium Mkapa atakuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Mhe Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.
Post A Comment: