WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania bado inawahitaji wawekezaji zaidi katika sekta ya uzalishaji wa sukari ili iweze kukidhi mahitaji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Mauritius nchini Tanzania mwenye makazi yake Maputo nchini Msumbiji, Mheshimiwa Jean Pierre Jhumun, ofisini kwake jijini Dodoma.

“Mwaka jana nilikiwa nchini Mauritius nilihudhuria Jukwaa la Wafanyabiashara na Wawekezaji kati ya Tanzania na Mauritius, ambapo nilipata fursa ya kuwashawishi wawekezaji wa Mauritius waje kuwekeza kwenye viwanda vya sukari nchini,”.

Ameongeza kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya maeneo ya uzalishaji wa sukari ambayo bado hayajaendelezwa, hivyo kama kuna wawekezaji walio tayari na wamekidhi vigezo waendelee na hatua za uzalishaji.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa mbali na kuhitaji wawekezaji kwenye sekta ya sukari, pia amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Mauritius kuja kuwekeza kwenye sekta ya uvuvi. “Mnaweza kuja kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji wa samaki kwani tuna bahari, mito na maziwa yenye samaki wa aina mbalimbali,”

Kwa upande wake, Balozi Jhumun amesema wawekezaji wa Mauritius  wapo tayari kuwekeza katika uzalishaji wa sukari pamoja na uvuvi na wameshafanya utafiti katika baadhi ya maeneo.

Balozi Jhumun amesema ameambatana na Mwenyekiti wa Mfuko wa Uwekezaji wa Sukari,  Bw. Gansam Boodram kutoka nchini Mauritius kwa ajili ya kufuatilia maeneo ya uwekezaji.

“Tumeitikia wito wa Rais Dkt. John Magufuli wa  kututaka kusaidia katika upatikanaji wa wawekezaji watakaokuja Tanzania kuwekeza kwenye viwanda vya uzalishaji wa sukari,”.

Naye Bw. Boodram amesema tayari wameshatembelea baadhi ya maeneo wanayohitahi kwa ajili ya uwekezaji na wameshafanya utafiti wa udongo pamoja na masoko. Maeneo waliyoyafanyia utafiti ni Kasulu na Kibondo mkoani Kigoma pamoja na Rufiji mkoani Pwani.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 15, 2018.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: