Na Benny Mwaipaja, WFM, Kigoma
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmahauri ya Wilaya ya Kigoma kumrejesha mara moja katika kituo chake cha kazi cha awali, dereva wa Kituo cha Afya Bitale, kilichoko Kata ya Bitale katika Halmashauri ya wilaya hiyo baada ya kubainika kuwa gari la kubeba wagonjwa kituoni hapo halina dereva.
Dkt. Kijaji, ametoa maelekezo hayo alipotembelea Kituo hicho cha Afya kukagua ujenzi wa majengo mapya ya Kituo hicho yatakayogharimu shilingi 400m baada ya Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Bitale, Dkt. Norbert Nshemetse, kueleza changamoto ya upungufu wa watumishi wa kituo hicho akiwemo dereva.
Dkt. Nshemetse, pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuwapatia gari la wagonjwa (Ambulance) katika kituo hicho, alisema gari hilo halina dereva baada ya dereva wake kuhamishiwa katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma mwezi Julai, 2018.
"Katika jambo lililonishitua ni kupata taarifa kwamba dereva aliyekuwa akiendesha gari la wagonjwa hapa Kituoni amehamishwa kupelekwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wakati anahitajika zaidi hapa kuliko huko kwa Mkurugenzi" alisikitika Dkt. Kijaji
Alimwamwagiza Mkurugenzi Mtendaji huyo kumrejesha dereva huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja kituoni hapo ili aendelee na kazi ya kuwahudumia wagonjwa.
"Tunaposema thamani ya fedha ni pamoja na mambo haya, gari lipo lakini halina dereva. Mkurugenzi, mrejeshe dereva huyo hapa wewe tafuta dereva mwingine, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkuu wa Wilaya hebu lisimamie hili" aliagiza Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji, alitembelea Kituo hicho cha afya ambacho kimepata fedha kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba ikiwemo jengo la wazazi, maabara, jengo la kuhifadhia maiti, wodi ya watoto, nyumba ya mtumishi, jengo la mionzi, kliniki ya mama, baba na mtoto na kuweka mfumo wa teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA.
Hata hivyo ujenzi wa majengo hayo ulikuwa haujaanza na kumfanya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango kuagiza uanze mara moja kwa sababu fedha zipo kwenye akaunti ya Kituo hicho cha Afya ili lengo la Serikali la kuboresha huduma za afya kwa wananchi liweze kufanikiwa.
Post A Comment: