Mkuu wa Wilaya ya Geita Josephat Maganga akizungumza na mwanafunzi wa shule ya sekondari Kalangalala, Aron Mkono aliyelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Geita baada ya kupigwa na mwalimu wa nidhamu
Na Rehema Matowo, Mwananchi
Geita. Takribani wanafunzi 100 wa kidato cha tano na sita shule ya sekondari Kalangalala mjini Geita wameandamana kwenda ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Geita kupinga kitendo cha mwenzao kupigwa na mwalimu hadi kupoteza fahamu.
Wanafunzi hao leo Ijumaa Agosti 31, 2018 wametembea umbali wa kilomita 3 kwenda kwa mkuu huyo wa wilaya, Josephat Maganga.
Mwanafunzi huyo Jonathan Mkono amepigwa na mwalimu waliyemtaja kwa jina moja la Lawi jana Alhamisi Agosti 30, 2018 kwa kosa la kuingia bwenini wakati vipindi vikiendelea.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake mbele ya mkuu huyo wa wilaya na kamati ya ulinzi na usalama, mwanafunzi, Aron Mathias amesema hali ya mwenzao aliyelazwa hospitali ya mkoa si nzuri, kwamba hawezi kuzungumza, kukaa wala kusimama.
"Huyu ni kiongozi alikua anasimamia usafi alivyomaliza alirudi bwenini kuchukua vifaa lakini mwalimu Lawi alimwadhibu na sio kwa fimbo alimpiga makofi na marungu,” amesema.
Mwanafunzi huyo amedai baada ya kipigo mwenzao alipoteza fahamu na baadaye alizinduka lakini hali yake ilikuwa mbaya na usiku walilazimika kukodi pikipiki kumpeleka hospitali.
“Tulimpeleka hospitali akiwa mahututi tulipofika daktari alikataa kumpokea akishinikiza kupewa taarifa ya polisi , tulivyoipata ndio wakaanza kumtibu majereha yake,” amesema.
Kwa upande wake Maganga amewasikiliza na kuwataka kurudi shule ambako ataenda na kufanya kikao na wanafunzi pamoja na walimu.
Chanzo- Mwananchi
Post A Comment: