Zaidi ya Waislamu milioni mbili kutoka duniani kote wameanza leo kuhudhuria ibada ya hija katika maeneo takatifu ya Kiislamu nchini Saudi Arabia. Hayo ni wakati Saudia na Qatar zikiendelea kuzozana kidiplomasia.
Nchi hiyo ya kifalme ambayo ni ya kihafidhina zaidi, na ambayo inafanya mageuzi makubwa ya kijamii na kiuchumi, imekusanya raslimali nyingi kwa ajili ya kufanikisha ibada hiyo ya siku sita, ambayo ni mojawapo ya nguzo tano za Uislamu.
Ijapokuwa mrithi wa ufalme Mohammed bin Salman, ameongoza mageuzi katika taifa hilo la kifalme, dini inasalia kuwa nguvu muhimu nchini humo.
Nchi hiyo iliondoa mwezi Juni marufuku ya wanawake kuendesha magari na imeongeza nafasi za kazi kwa wanawake katika jamii inayotawaliwa na wanaume.
Lakini mageuzi hayo yameandamana na msako mkubwa dhidi ya wapinzani, ambapo wanaharakati kadhaa wa haki za wanawake wamezuiwa katika wiki za karibuni. Wengine wameachiwa huru.
Wakati huo huo, Qatar imeilaumu Saudi Arabia kwa kuwazuia raia wake kuhudhuria hija ya mwaka huu kutokana na mzozo wa kidiplomasia unaoendelea kati ya nchi hizo mbili. Serikali ya Saudi Arabia hata hivyo imekanusha hayo na kusema Waqatari bado wanasafiri kuelekea Mecca.
Katika mpango wa kuzuia idadi kubwa ya Waqatari kuingia nchini humo Saudi Arabia ilikuwa imewakubalia Waqatari 1,200 pekee kuhudhuria hija ya mwaka huu ila Qatar inasema raia wake hawajaweza kupata vibali vya kuingia
Qatar inalaumu suala hilo kutokana na mzozo wa kidiplomasia na majirani zake wa Ghuba - Saudi Arabia, nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri. Shirika la kutetea haki za binadamu la Qatar limesema Saudi Arabia iliufunga mfumo wa kuwasajili watu kielektroniki ambao unatumiwa na mashirika ya usafiri kupata vibali kwa mahujaji wa Qatar. Afisa wa Saudi Arabia amekanusha madai hayo na kuilaumu Qatar akisema wao ndio waliozuia njia hiyo ya usajili.
Post A Comment: