Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abdallah Chikota.

 Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imewatimua kwenye kikao viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kwa kushindwa kuwasilisha majibu ya hoja za jumla ya Sh. milioni 371 zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2016/17.

Kufuatia hatua hiyo, viongozi hao wametakiwa kuandaa upya kitabu cha majibu ya hoja hizo kwa gharama zao na kukiwasilisha tena kwa kamati kwa muda utakaopangwa.

Hali hiyo ilijitokeza jana katika kikao cha kamati hiyo cha kufanya mahojiano na halmashauri hiyo kuhusu hoja za ukaguzi za mwaka huo kutokana na kamati kushindwa kuendelea na mahojiano hayo na kuitimua.

Akizungumzia hatua hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abdallah Chikota alisema wameirudisha kuandaa upya majibu ya hoja hizo kutokana na upungufu ulioonekana kwenye kitabu kilichowasilishwa kwenye kamati hiyo.

Alisema kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, kamati hizo za Hesabu za Umma ya LAAC na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (PAC), zinafanya majadiliano kulingana na taarifa za CAG.

"Katika hesabu za mwaka 2016/17 kuna hoja kadhaa zimejitokeza kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na tulitarajia leo (jana) watakuja na majibu, lakini kilichofanyika kwenye kitabu chao hawakuweka majibu wakaelekezwa na ofisi ya CAG kule Mara kwamba kitabu chao kina upungufu, hata hivyo hawakuweka,"alisema.

Aliongeza: "Wakaitwa na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) kufanya kikao cha maandalizi wakaambiwa kitabu kina dosari, lakini bado hawajaweka hayo majibu na leo wametokea kwenye kamati yetu wakiwa na upungufu huo huo, sisi hatuwezi kuendelea na majadiliano kwa sababu hatujui matumizi ya fedha hizo zilizooneshwa kwenye hoja za CAG."

Chikota ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Nanyamba (CCM), alisema miongoni mwa fedha ambazo hawajapata majibu ni Bakaa ya Sh. milioni 186 za Mfuko wa wahisani katika kuboresha huduma za afya (Basket Fund).

"Wangeleta majibu ya hizi fedha tungepima uzito wa majibu yao wametumia kwa matumizi gani, pia kuna matumizi yasiyotakiwa ya Shilingi milioni saba, tumeambiwa kwenye mradi wa maji kuna Bakaa ya Sh. milioni 26, tujue kama fedha zimetumika,"alisema.

Makamu Mwenyekiti huyo alisema kamati hiyo imefungwa mawanda ya kuhoji kilichojiri kutokana na kukosekana majibu.

"Kwenye akaunti ya maji kuna fedha Shilingi milioni nne zimetumika kwa shughuli ambazo hazikufanywa, yaani waliidhinisha malipo ya fedha hiyo kwa shughuli ambayo haijafanywa,"alisema.

Kadhalika, alisema katika Mfuko wa barabara kuna malipo yana dosari ya Sh. milioni 124, fedha za Tasaf Sh. milioni 24, zilitakiwa kurejeshwa makao makuu hazijarejeshwa na majibu hakuna.

"Kwa mazingira haya tumewafukuza wakaandae tena kitabu kwa gharama zao, maana hawawezi tena kutumia fedha za umma kwa ajili ya kuleta majibu ambayo walitakiwa kuleta kwa kipindi hichi na tutafuatilia kama mtalipana tena posho,"alisema.

Alimtaka RAS kuhakikisha anasimamia maandalizi ya kitabu kipya cha majibu ya hoja hizo na kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) watajulishwa siku ya kukutana na kamati.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Josephat Kandege, alisema wamepokea maelekezo ya kamati na watahakikisha wanasimamia na majibu yatapatikana.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: