Siku chache baada ya mkuu wa wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani, Mh. Jokate Mwegelo kufanya oparesheni ya kukata mifugo katika maeneo ya hifadhi zilizopo wilayani humo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina amepiga marufuku tabia ya ukamataji mifugo kiholela.

Mpina ametoa marufuku hiyo wakati akifunga maonesho ya 25 ya Nane nane Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro katika viwanja vya Mwalimu JK Nyerere mjini Morogoro.

Mpina amesema katika siku za hivi karibuni kumeibuka tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali kuendesha operesheni za kukamata mifugo na kuifungia bila kuipatia huduma muhimu ikiwemo maji, malisho na matibabu na matokeo yake mifugo mingi hufa na kusisitiza kuwa operesheni hizo zinapofanyika ni lazima zihusishe pia maofisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuwa na uelewa wa pamoja wa jambo hilo.

Aidha Mpina alisema utaratibu unaofanyika hivi sasa wa kukamata hovyo mifugo ni ukiukwaji wa sheria namba 17 ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003 na, Sheria ya Ustawi wa Wanyama Namba 19 ya Mwaka 2008 ambazo zinataka mifugo inapokamatwa kuzingatia masuala ya magonjwa na ustawi wa mifugo katika kipindi chote inapokuwa imeshikiliwa.

Katika hatua nyingine, Mpina pia alielezea kutoridhishwa na utoaji wa mikopo wa Benki ya Kilimo (TADB) ambapo kwa taarifa iliyotolewa sekta ya uvuvi hakuna mkopo wowote uliotolewa katika mwaka wa fedha uliopita huku upande wa sekta ya mifugo wakiambulia wajasiamali wanne tu .

Aidha kiasi cha jumla ya mikopo iliyotolewa ya Sh. Bilioni 39 kwa mwaka mzima ni kidogo sana ikilinganishwa na mahitaji wa mikopo katika sekta za kilimo,mifugo na uvuvi, huku akipongeza kazi nzuri inayofanywa na Taasisi ya PASS na SAGGOT-CTF katika kuwadhamini wakulima , wafugaji na wavuvi katika kupata mikopo.

Kutokana na changamoto hizo, Waziri Mpina ameitaka benki hiyo kurekebisha kasoro zilizopo na kujipanga vizuri kuhudumia sekta hizo, vile vile amewaagiza makatibu wakuu wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuitambua na kupitia miradi yote ya wajasiriamali katika sekta zao ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa wakati.

Sambamba na hilo amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kupitia idara ya maendeleo ya jamii na idara ya ushirika kuwaandaa na kuwaunganisha wananchi katika kukidhi vigezo vya kupata mikopo katika taasisi za fedha.

Pia aliagiza Halmashauri zote nchini kuwatambua vijana wanaohitimu mafunzo katika vyuo vya ugani vya SUA, FETA, LITA na ATI na kuwatumia katika safari ya kuleta mageuzi ya uvuvi,mifugo na kilimo katika maeneo yao na kwamba hata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake,vijana na walemavu kundi hili la wagani liangaliwe kwa jicho la pekee.

Mbali na hilo Waziri Mpina alisema pamoja na Serikali kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa mialo na masoko ya samaki baadhi ya halmashauri zimetelekeza miundombinu hiyo na kuendelea kutoa huduma katika maeneo yasiyo rasmi, pia baadhi ya mialo na masoko haifanyiwi matengenezo wala ukarabati kiasi cha kukosa huduma muhimu kama maji, vyoo, umeme na majokofu ya kuhifadhia samaki hali inayosababisha usumbufu na hasara kwa wananchi licha ya kutozwa ushuru kila uchao.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mpina ametoa miezi mitano kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinakarabati na kuweka huduma muhimu na kwamba wataoshindwa kufanya hivyo mialo na masoko hayo yatarejeshwa chini ya usimamizi wa Wizara na halmashauri hizo hazitaruhusiwa tena kukusanya mapato yatokanayo na sekta hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alimhakikishia Waziri Mpina kuwa maagizo yote aliyotoa watayafuatilia na kuyasimamia ili kuona utekelezaji wake kwani Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuleta mageuzi ya kweli katika sekta za Kilimo,Mifugo na Uvuvi.

Pia Ndikilo alisema ni jambo la kusikitisha kuona licha ya fursa kubwa za mifugo na uvuvi zilizoko katika mikoa ya Kanda ya Pwani lakini hadi sasa hakuna kiwanda hata kimoja cha kuchakata samaki wala nyama na kumuomba Waziri Mpina kuandaa kongamano ya mikoa hiyo ili kujadili kwa pamoja namna ya kuwekeza katika viwanda vya kuchakata bidhaa hizo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Stephen Kebwe alisema maonesho hayo ya mwaka huu yamekuwa na mafanikio makubwa kwani wakulima,wafugaji na wavuvi na makundi mengine yamejitokeza kwa wingi na wamepata fursa ya kujifunza teknolojia mpya zitakazoboresha uzalishaji.

Maonesho hayo yalihudhuriwa na wakuu wa mikoa, wilaya, mameya, wakurugenzi wa halmashauri,madiwani pamoja na sekta binafsi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: