Serikali ya CCM katika awamu ya tano chini ya uongozi wa Mhe Dkt John Pombe Magufuli, imejidhatiti katika mwaka huu wa fedha  2018/2019  kukamilisha miradi  ya maendeleo katika sekta ya Afya ambayo haikukamilika katika awamu iliyopita ikiwemo miundo mbinu ya majengo pamoja na Vifaa tiba wilayani Nyamagana.

Haya yamebainishwa na Mbunge Jimbo la Nyamagana Mhe Stanslaus Mabula alipokuwa kwenye ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo  katika Kata tatu Isamiro, Pamba pamoja na Kata ya Mahina. Ambapo katika mwaka huu wa fedha 2018/2019 serikali imetenga shilingi . 261,000,000 kukamilisha ujenzi wa Zahanati katika kata hizi tatu.

Mhe Mabula amepata fursa ya kutembelea Zahanati ya Mahina ambayo imepewa shilingi 87,000,000 kukamilisha Wodi mbili ya Wanaume, Mama na Mtoto pamoja na eneo la kupumzikia, vyumba vinne ikiwa ni Chumba cha kujifungulia, chumba  cha kupumzika  baada ya kujifungua na vyumba vinavyobakia ni kwaajili ya Madaktari na wahudumu wa Afya.

Mhe Mabula kadharika ametembelea Kata ya Pamba ambayo imepatiwa shilingi 67,000,000 kukamilisha ujenzi wa wodi Wanaume, Mama na Mtoto pamoja na Chumba cha kujifungulia na mapumziko baada ya kujifungua katika Zahanati ya Bugarika. Kisha akakamilisha ziara yake leo kwa kukagua Zahanati ya Isamiro iliyopatiwa shilingi 107,000,000 kukamilisha ujenzi wa jengo la Zahanati ya Isamiro ambayo ujenzi wake ulianza toka mwaka 2014.

"Mwaka 2015 niliweka ahadi kwa wananchi kukamilisha miradi yote ambayo haikuwa imekamika katika awamu zilizopita. Ninafarijika kuona mwaka 2018 tunakamilisha viporo vyote vya ujenzi wa Zahanati na Vifaa vyake vyote". Mhe Mabula amesema.

Ziara ya Mbunge kesho itaendelea katika kata ya Mhandu na Mkuyuni.

Imetolewa na
Ofisi ya  Mbunge
Jimbo la Nyamagana🇹🇿
Share To:

msumbanews

Post A Comment: