Hussein Makame, NEC-Dodoma
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo matatu na wa udiwani katika kata mbili za Tanzania Bara utakaofanyika Septemba 16, mwaka huu.

Akitangaza uchaguzi  huo mjini Dodoma leo, Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mbarouk Salim Mbarouk alisema fomu za uteuzi wa wagombea wa Majimbo hayo zitatolewa kuanzia tarehe 13 hadi 20 Agosti, mwaka huu na uteuzi utafanyika tarehe 20 Agosti, 2018 wakati kampeni zitaanza zitaanza tarehe 21 Agosti,  na kumalizika tarehe 15 Septemba, mwaka huu.

Jaji Mbarouk alisema “Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Ubunge katika Majimbo matatu”

Aliyataja majimbo hayo kuwa ni Korogwe Vijijini, Mkoa wa Tanga kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Ndugu Stephen Hilary Ngonyani, Jimbo la Ukonga Katika Mkoa wa Dar Es Salaam na Jimbo la Monduli katika Mkoa wa Arusha

Alisema wabunge wa majimbo hayo mawili Ndugu Mwita Mwikabe Waitara na Ndugu Julius Kalanga Laizer wajiuzulu uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na hivyo kupoteza sifa za kuwa Wabunge.

“Baada ya kupokea taarifa hizo na kwa mujibu wa vifungu vya 37 (1) (b) na 46 (2) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatoa taarifa kwa Umma kuwa majimbo matatu ya Korogwe Vijijini, Ukonga na Monduli yapo wazi”, alisema.

Katika hatua nyingine, Jaji Mbarouk alisema kwa kuzingatia masharti ya vifungu vya 37(1)(b) (5) na 46 (2) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Tume inatoa taarifa wa Umma kuhusu Ratiba ya uchaguzi mdogo katika majimbo hayo.

Aliongeza kuwa Tume pia inatoa taarifa kwa umma kuwa uteuzi, Kampeni na uchaguzi wa  Madiwani kwa Kata za Tindabuligi na Kisesa katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu uliohirishwa hapo awali utafanyika sambamba na ratiba ya Uchaguzi Mdogo  wa ubunge katika Majimbo hayo matatu.

“Tume inachukua nafasi hii kuvikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maelekezo yote wakati wa kipindi cha uchaguzi mdogo wa Majimbo hayo matatu na hizo Kata mbili” alisema.

Uchaguzi huu mdogo wa majimbo matatu na kata mbili za Tanzania Bara, unafuatia uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Buyungu unaotarajiwa kufanya Agosti 12 pamoja na kata 37 za Tanzania Bara.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: