Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka Wasimamizi wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika Septemba 16 mwaka huu katika Majimbo ya Ukonga na Monduli na kwenye Kata 13 za Tanzania Bara kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria na Kanuni zinazosimamia uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa), Semistocles Kaijage ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi wa Kata na Majimbo hayo.

Jaji Kaijage amewataka Wasimamizi hao kuzingatia weledi na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ili wapunguze na kuondoa malalamiko yanayojitokeza wakati wa uchaguzi.

Amesema  Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa akisisitiza kwamba hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri wenye ufanisi usio na malalamiko au vurugu.


“ Tunakutana hapa kwa muda wa siku tatu (3) ili kwa pamoja tubadilishane uzoefu, tujadili namna ya kufanikisha zoezi la uchaguzi lakini pia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi,” Amesema Jaji Kaijage.


Aidha, amewataka Wasimamizi hoa waepuke madhara yanayotokana na ukiukaji wa Sheria, Kanuni na taratibu za Uchaguzi  na akisisitiza kwamba katika kipindi hiki chaguzi  zinafanyika katika mazingira ambayo yana hamasa kubwa ya Kisiasa, kutoaminiana na wakati mwingine hutawaliwa na mihemko ambayo imekuwa chanzo cha ufunjivu wa amani.

Jaji Kaijage amewaeleza Wasimamizi hao kwamba wameaminiwa na kuteuliwa katika nafasi hizo za usimamizi wa Uchaguzi kwa kuwa wana uwezo wa kufanya kazi hiyo hivyo wajiamini na kujitambua.

Amaetoa wito kwa Wasimamizi hao kuhakikisha kuwa wanayaelewa vema maeneo yao ya kazi na kuhakikisha kwamba wanawatumia vizuri wasaidizi walio nao katika maeneo yao kwa matokeo bora.

“Mjue mna jukumu la kuimarisha imani ya wananchi pamoja na wadau wote wa uchaguzi kwa Tume. Hivyo mfanye kazi kwa ufanisi wa hali ya juu, bila kuegemea upande wowote. Kufanya kazi kwa uhuru na kwa uwazi kutasaidia kudumisha amani katika maeneo yenu ya Uchaguzi” Amesisitiza.

Kuhusu kufanyika kwa Uchaguzi huo mdogo Septemba 16 mwaka huu,  Jaji Kaijage amesema kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 kikisomwa pamoja na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura 292, ni jukumu la Tume kusimamia, kuendesha na kuratibu uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi.

Amesema kwa nyakati tofauti Tume imepokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kuzingatia Kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Ubunge katika Majimbo ya Ukonga, Korogwe Vijijini na Monduli.

Pia amefafanua kuwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, ambaye kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali ya Mitaa, Sura, 292 alitoa taarifa ya uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 23 kutoka katika Halmashauri 15 zilizopo katika Mikoa 10 ya Tanzania Bara.

Aidha, katika uchaguzi huu mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika Septemba 16 mwaka huu Mgombea Ubunge katika Jimbo la Korogwe Vijijini amepita Bila Kupingwa na jumla ya wa wagombea 10 wa Udiwani katika Kata 10 wamepita bila Kupingwa, hivyo jumla ya Kata zilizobaki zitakazoingia kwenye uchaguzi mdogo ni 13 na Majimbo 2 ya Monduli, Arusha na Ukonga jijini Dar es salaam.

MWISHO
Share To:

msumbanews

Post A Comment: