Picha haihusiani na tukio.

Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Msingi Kibeta iliyoko Manispaa ya Bukoba, Sperius Eradius (13), amefariki dunia akidaiwa kupigwa na mwalimu wake akituhumiwa kuiba pochi ya mwalimu.

Baadhi ya wanafunzi walioshuhudia tukio hilo lililotokea jana, waliiambia Nipashe kuwa mwanafunzi huyo alikwenda kumpokea mizigo mwalimu wake aliyefika shuleni hapo kwa usafiri wa bodaboda, lakini baada ya kuingia ofisini alianza kulalamika kutoiona pochi yake.

Wanafunzi hao walidai mwanafunzi mwenzao aliitwa na kuanza kuhojiwa kuhusu kupotea kwa pochi hiyo na akakana kuichukua, hali iliyosababisha kuanza kupigwa akitakiwa kuirejesha.

Wamesema kuwa baadaye walitakiwa kuitafuta pochi hiyo mpaka chooni, lakini hawakuiona huku mwanafunzi huyo akiendelea kuadhibiwa.

 Hata hivyo, ilielezwa na wanafunzi hao kuwa wakati mwanafunzi mwenzao akiendelea kupigwa, dereva bodaboda alifika shuleni hapo akimtafuta mwalimu aliyepoteza pochi na kumkabidhi pochi aliyokuwa ameisahau kwenye pikipiki yake.

Mashuhuda hao walisema kuwa baada ya pochi hiyo kupatikana, mmoja wa walimu aliagiza mwanafunzi huyo apatiwe juisi na bagia, chakula ambacho hakuweza kukila kutokana na maumivu, hata hivyo.

Ripoti ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kagera, Dk. John Mwombeki, alikiri kupokea mwili wa mtoto huyo majira ya saa mbili asubuhi ukionekana kuwa na majeraha ya siku za nyuma. Dk. Mwombeki amesema uchunguzi wa awali wa mwili wa mtoto huyo ulionyesha amefariki dunia kutokana na kipigo.

Juni 16, 2018 katika kilele cha siku ya Mtoto wa Afrika, ambayo kitaifa ilifanyika mkoani Arusha na Tanzania ikitajwa kuongoza katika vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kuliko uovu unaofanywa kwenye ujambazi, takwimu zilizowasilishwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , Dk. Faustine Ndugulile, zinaeleza kuwa watoto 41,000 walifanyiwa ukatili kati yao 3,467 kwa kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana.

Lakini pia, Idara ya Ustawi wa Jamii wizarani hapo, ilieleza kuwa asilimia 60 ya ukatili dhidi ya watoto unafanyika nyumbani, asilimia 35 ni shuleni na iliyobaki ni maeneo mengine.

Chanzo: Nipashe
Share To:

Anonymous

Post A Comment: