Familia ya Bwn. Khakoo ikimkabidhi vifaa tiba Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Prf. Lawrence Museru mapema leo , kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa huduma za uuguzi Sista Zuhura Mawona


Baadhi ya vifaa tiba (Screen) ambavyo hutumika kumsitiri mgonjwa wakati akipatiwa huduma. 


Pichani ni vifaa tiba vilivyokuwa chakavu kabla ya kufanyiwa matengenezo na familia hiyo. 
Prof. Museru akiwa katika picha ya pamoja na familia ya Bwn. Khakoo na baadhi ya wakurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili. 


Bwn. Khakoo akimuelezea Prof. Museru jinsi walivyofanyia matengenezo vifaa hivyo

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea vifaa tiba 69 ambavyo vimefanyiwa matengenezo na kurejea katika viwango vyake vya matumizi. 

Vifaa tiba hivyo (Screen) ambavyo vilikua chakavu vimetengenezwa upya na familia ya Bwn. Khakoo bila malipo yoyote, ambavyo hutumika kumsitiri mgonjwa akiwa kitandani huku akipatiwa huduma hospitalini na kwamba matengenezo yake yamegharimu shilingi milioni 2. 7. 

Katika matengenezo hayo familia ya Khakoo imejitolea kulipa wafanyakazi , kununua vitambaa pamoja na mashono huku MNH ikiunga mkono jitihada hizo kwa kutoa mashine ya kuchomelea na vifaa vya kupakia rangi. Akipokea vifaa tiba hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru ameishukuru familia ya Bwn. Khakoo kwa msaada huo na kueleza vifaa hivyo ni muhimu kwa kutolea huduma hospitalini hivyo vitatumika kwa uangalifu. 

‘‘Tunashukuru sana kwa msaada huu mkubwa kwakweli tumejifunza kwamba vifaa vilivyochakaa vinaweza kutengenezwa upya na vikakutumika tena, hili tumelichukua na tutalifanyia kazi kadiri  inavyowezekana’’.Amesema Prof. Museru. Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa huduma za uuguzi, Sista Zuhura Mawona amesema kila wodi inahitaji screen 6 ambazo hutumika kumsitiri mgonjwa wakati akihudumiwa hivyo zitagawiwa kulingana na mahitaji. 

Kwa upande wao familia ya Bwn. Khakoo imesema wameamua kutengeneza vifaa hivyo kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano ya kuboresha huduma za afya nchini na kutoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huo. 

‘‘ Tuliviona vifaa hivi vikiwa chakavu tukaona kwamba kuna uwezekano wa kuvitengeneza na vikaendelea kutumika kwa wagonjwa , sisi ni watu binafsi tumeamua kama familia kujitolea na hivyo tumeokoa fedha nyingi takribani shilingi milioni 30. Amesema Bwn. Khakoo. Vifaa hivyo endapo vingenunuliwa vipya kimoja kingegharimu shilingi laki nne hadi laki tano.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: