Mkuu mpya wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya amesema atashughulika na watu wote ambao wanamtukana Rais John Magufuli wilayani humo.
Ole Sabaya ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Sambasha, wilayani Arumeru mkoa wa Arusha alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kumpongeza kwa kuteuliwa kwake mwishoni mwa mwezi uliopita kushika wadhifa huo.
Amesema wakati Rais akihangaika na shida za wananchi ili kupunguza ukali wa maisha wapo baadhi ya watu ambao hakuwataja majina wilayani Hai na katika maeneo mengine wamekuwa wakimtukana Rais ikiwa ni pamoja na kudai anabagua Kanda ya Kaskazini.
“Mheshimiwa Rais amenichagua katikati ya watu milioni 50, akanifanya kuwa Mkuu wa Wilaya, kama hayo maneno yanayosemwa kuwa Rais anabagua kanda hii lakini mimi nimekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai leo, akamchagua Jerry Muro anayetokea Hai (Machame), kama Rais anabagua kama wanavyodai Mungu na aamue sasa.
“Lakini kabla hajaamua hayo maneno yalisemwa Hai tena kanisani, ila naamini ana taarifa na hatarudia tena kufanya uzembe wa namna hiyo kwenye Wilaya ya Hai, hatarudia maneno hayo ya kuchonganisha Serikali na wananchi, Rais anahangaika na viwanda, kupunguza ukali wa maisha na kuwaondolea wananchi tabu na dhiki, anayechukua mamilioni ya fedha kujinufaisha anakwenda kumtukana Rais naamini hatafanya hivyo tena,” amesema Ole Sabaya.
Naye Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma, aliwataka wananchi kutodanganywa na propaganda za ubaguzi zinaoenezwa zikidai Rais hapendi watu wa Kanda ya Kaskazini.
“Watanzania hatuna ubaguzi, tukemee hilo pepo la ubaguzi uwe wa kabila au dini, mimi nilimtengeneza Rais nikiwa Mwenyekiti wake wa mkoa, najua ukishughulika na maisha ya wanyonge lazima mabepari yakushughulikie, nimekaa bungeni miaka miwili na nusu na simjui mbunge wenu anaitwa nani, anaongeaga kweli hata bungeni? alihoji Musukuma.
“Kwa kuwa ninyi mna lami kila sehemu hana haja ya kuongea, kwa barabara za shida hizi, Ole Sabaya atashughulika na hili jimbo mimi nakwambia kama King, pamoja na ukuu wa wilaya lakini piga kazi mwaka 2020 tutakuja kukuombea kura Mungu akipenda, hii ndiyo safari na wakati mchungaji anaomba nilikuwa nasikiliza nikafikiri anataka kusema hili akaogopa ila mi nasema mchungaji amekuombea ubunge,” aliongeza.
Post A Comment: