Mkuu mpya wa wilaya Nyamagana Mhe. Dkt.
Philis Misheck Nyimbi (kulia) akila kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa Mwanza
Mhe. John Mongella (kushoto). Mhe. Dkt. Nyingi amechukua nafasi ya
Mhe.Marry Tesha.
Judith Ferdinand Mwanza.
Wakuu wa wilaya zote mkoani Mwanza wametakiwa kutimiza vyema majukumu
yao na kuhakikisha kuna ukusanyaji na usimamiaji madhubuti wa mapato.
Mkuu wa mkoa Mwanza Mhe.John Mongella ametoa agizo hilo leo wakati
akiwaapisha wakuu wapya wa wilaya za Nyamagana, Ilemela, Magu na Ukerewe
walioteuliwa hivi karibuni na Rais Dkt.John Pombe Magufuli.
Mhe.Mongella alibainisha kwamba katika majiji sita nchini, Jiji la
Mwanza ni la tani kwa ukusanyaji wa mapato huku Manispaa ya
Ilemela
ikishika nafasi ya tatu kutoka mwisho miongoni mwa Manispaa zote.
Aidha Mhe.Mongella aliwasisitiza wakuu hao wa wilaya kufanya kazi kwa
uadilifu huku wakifuata misingi ya kazi kwa kuhakikisha ulinzi,
usalama, utulivu na kuhamasisha maendeleo katika wilaya zao.
Mkuu wa wilaya Ilemela, Mhe. Dkt. Severine Lalika alimshukuru Rais
Dkt.Magufuli kwa kumteua katika nafasi hiyo na kuahidi ushirikiazo na
viongozi mbalimbali katika kutatua kero na kuleta maendeleo kwa wananchi
wa wilaya hiyo.
“Mtu mmoja hawezi kuleta maendeleo, hivyo nitashirikiana na Manispaa
ya Ilemela akiwemo Mkurugenzi na baraza la madiwani kwenye vipaumbele
vyao kwani naamini ndipo changamoto na kero za wananchi zilipo, pamoja
na kamati ya ulinzi na usalama ili kuhakikisha wilaya inakuwa salama”.
Alisema Mhe.Dkt. Lalika.
Naye mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mhe. Dkt. Philis Nyimbi alisema ili
waweze kufanya kazi vizuri ataendeleza mikakati mizuri iliyopo na
kuongeza mikakati mipya huku akisimamia vyema ajenda ya viwanda kwa
kuendeleza vilivyopo na kuanzisha vipya pamoja na kutumia taaluma yake
kuwasaidia wananchi wa wilaya hiyo katika sekta ya afya.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya Magu Mhe. Philemon Sengati aliahidi
kufanya kazi kwa bidii huku akishirikiana na viongozi mbalimbali katika
kutatua kero za wananchi wa wilaya hiyo hususani maji, kilimo na
ufugaji.
Aidha mkuu wa wilaya Ukerewe, Mhe. Cornel Magembe alisema ataitumikia
nafasi hiyo kwa kasi anayohitaka Rais Magufuli na kuahidi kupambana na
suala la uvuvi haramu katika visiwa vyote 32 vya wilaya hiyo.
Post A Comment: