Mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja amekanusha habari zilizoandikwa na moja ya magazeti hapa nchini wiki iliyopita zikidai amestaafu mambo ya siasa.
Mgeja ambaye mnamo mwaka 2015 yeye na baadhi ya wana CCM wengine walikihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA, alikanusha habari hizo leo mbele ya baadhi ya wazee na waumini wengine wa kiislamu wakati wa hafla ya chakula alichokiandaa kwa ajili ya kusherehekea sherehe za Idd el Hajj.
Akifafanua kuhusu taarifa hizo, Mgeja alisema kukaa kwake kimya bila kujihusisha na masuala ya kisiasa kwa hivi sasa haimaanishi ameachana na siasa na kwamba kukaa kimya ni dawa tosha ya kuwajibu watu na kwamba yeye bado atajihusisha na mambo ya kisiasa na yuko imara.
Aliendelea kueleza kuwa mpaka hivi sasa haelewi gazeti hilo katika toleo lake la Jumapili iliyopita lilizipata wapi habari hizo za kudai ameamua kustaafu siasa na kwamba sasa anajishughulisha na masuala ya kilimo kwa lengo la kuwa mmoja wa wakulima wakubwa hapo baadae.
“Ndugu wazee wangu na waumini wengine wa kiislamu mliokusanyika hapa leo kwa ajili ya kusherehekea sherehe ya Idd el Hajji, naomba nitumie fursa hii kupitia kwenu kukanusha habari zilizoandikwa na moja ya magazeti hapa nchini zikidai nimestaafu siasa,”
“Nakanusha habari hizo siyo za kweli na binafsi bado sijastaafu siasa kama ilivyoelezwa, maana hata kama nitafanya shughuli za kilimo, bado nitafanya siasa, tukumbuke hayati baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa akisema, Siasa ni kilimo,” alieleza Mgeja.
Alieleza kuwa anahisi watu waliosambaza habari hizo ni miongoni mwa mahasimu wake wakiwa na lengo la kuwakatisha tamaa jamaa zake wanaounga mkono katika harakati mbalimbali za kiuchumi na kisiasa kuona zinasimama katika misingi ya haki na usawa.
“Huenda nimekaa kimya kwa muda mrefu bila ya kutoa neno la kuuhabarisha umma wakadhani nimestaafu siasa, nawaomba watambue kuwa, Ukimya nao ni dawa tosha ya kuwajibu, nawathibitishia bado niko imara katika mapambano ya kutafuta haki kwa misingi ya sheria wala sijateteleka, sina wa kumuogopa,”
“Na kama ni suala la kilimo ni kweli maisha yangu yote najishughulisha na kilimo na ni katika kumuenzi mkono hayati baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, mara kwa mara alikuwa akisema, Siasa ni kilimo, hivyo huwezi kuachanisha siasa na kilimo, ni vitu viwili pacha,” alieleza Mgeja.
Alisema mtu mwenye uelewa mpana hawezi kustaafu kitoto toto kutoka kwenye siasa na kwamba wakati huu ni muhimu kwa watanzania kuliko wakati wowote tangia Tanzania ipate uhuru wake hivyo ni muhimu wana siasa wakasimama imara kuwasemea na kuwatetea watu.
Alisema yeye binafsi bado anaungana na wapenda demokrasia wenzake wanaoitakia mema nchi ya Tanzania kwa kuhakikisha demokrasia ya kweli inaimarika hapa nchini na kuona uhuru, haki na utawala wa kisheria unastawika ili watanzania wote wafaidi matunda ya demokrasia.
Aliendelea kueleza kuwa katika masuala ya kisiasa, hakuna mtu mwenye hatimiliki, na kwamba yeye binafsi ataendelea kufanya siasa na kupigania haki za msingi za kikatiba kwa watanzania ili kuhakikisha demokrasia ya kweli yenye misingi ya haki ya usawa inapatikana sambamba na kuishauri ama kuikosoa serikali.
Na Suleiman Abeid - Malunde1 blog
Post A Comment: