Bobi Wine

Timu ya mawakili 24 wameungana kumtetea Mbunge wa Kyadondo, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, huku wakimtaka Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu nchini Uganda, Med Kaggwa kuhakikisha anatumia vyema haki ya kikatiba ili kuhakikisha haki inatendeka.

Mbunge huyo anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Kijeshi siku ya Alhamisi kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria, ambapo hadi sasa Bobi Wine anashikiliwa kwenye gereza la Makindye ambalo ni la kijeshi huku akidaiwa kuwa hawezi kutembea wala kuzungumza.

Hata hivyo madai hayo ya Bobi Wine kuwa amepigwa na hali yake ni mbaya yalikanushwa na rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye aliziita kuwa ni habari feki na kusema " Mjukuu wangu Bobi Wine yupo salama na hali yake ni njema."

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za vyombo vya habari, mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki ana matatizo ya figo ambayo yanahitaji kutibiwa ipasavyo na madaktari bingwa waliobobea.

Mwanasheria wa mbunge huyo Male Mabirizi amefungua kesi Mahakama Kuu kutaka kuachiwa kwa mbunge huyo na wenzake wakiwamo wanaharakati mbalimbali waliokamatwa kwenye tukio la ghasia zilizoibuka wakati wa kufunga kampeni za ubunge wa Arua.

Mwanasheria huyo amedai kuwa Bobi Wine amechomwa sindano yenye dawa ambayo inamfanya asijitambue na mpaka sasa hajitambui wala uso wake hautambuliki pia pua na masikio vinatoka damu na kudai kuwa taarifa iliyotolewa na madaktari wa jeshi hazikuwa na ukweli.

Wiki iliyopita Bobi Wine na wenzake walishtakiwa baada ya kukamatwa wakiwa katika kampeni za kuelekea uchaguzi mdogo eneo la Arua kaskazini mwa nchi ambapo polisi wanasema walikuwa wamewaongoza wafuasi wao kushambulia msafara wa Rais Yoweri Museveni.

Hapo jana Jeshi la Polisi Uganda liliwashikilia watuhumiwa 45 katika vituo mbalimbali vya polisi kwa kufanya maandamano Jijini Kampala ya kupinga kushikiliwa kwa mbunge Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine na wabunge wenzake wanne.
Share To:

Anonymous

Post A Comment: