Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mhandisi Charles Kabeho amegoma kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa majengo ya kituo cha afya Kambarage katika Manispaa ya Shinyanga, mara baada ya kubainika kujengwa na matofali yaliyo chini ya kiwango.
Majengo yaliyobainika kujengwa chini ya kiwango ni matano ambayo ni wodi ya wazazi, wajawazito na watoto yaliyoanza kujengwa June 11 mwaka huu na kutarajiwa kukamilika Septemba 9, 2018 kwa gharama ya shilingi Milioni 500.
Akikagua majengo hayo jana Kabeho alibaini kuwa matofali yaliyojengwa yapo chini ya kiwango ambapo alianza kuyakagua kwa kuyavunja huku yakipukutika kama biskuti, ndipo aliposhtukia kuwa ujenzi wake umelipuliwa na hatimaye kugoma kuweka jiwe la msingi na kisha kuondoka.
“Matofali haya yapo chini ya kiwango hata ujenzi wa majengo mliyokwisha kujenga na mashaka nayo hayatadumu muda mrefu, yataanza kuchakaa na kuingizia hasara serikali hivyo sipo tayari kuweka jiwe la msingi kwenye mradi mbovu wa namna hii,”alisema Kabeho.
“Pia nimepata taarifa kuwa baadhi ya matofali mabovu kwenye mradi huu mlikuwa mmeshaanza kuyaondoa eneo hili yaani kuficha ushahidi, hivyo naagiza mfanye uchunguzi wenu kwa vipimo na ikibainika matofali yote yaliyojengwa ni mabovu bomoeni majengo yote,”aliongeza.
Pia alitoa wito kwa wafanyakazi wa serikali wakiwemo wahandisi kuacha kufanya kazi kiujanja ujanja ikiwa serikali ya awamu ya tano inataka watendaji wachapa kazi, wenye weledi na uzalendo na siyo wababaishaji.
Naye mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko alisema katika taarifa aliyopewa awali juu ya mradi huo hakuelezwa changamoto hizo za ubovu wa matofali, na hivyo kuagiza wale wote waliohusika kwenye majengo hayo watalipa gharama zote zilizotumika kwa kukatwa mishahara yao.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa manispaa ya Shinyanga (DMO) Lushajo Mwakajoka, alisema tatizo la matofali hayo kuwa chini ya kiwango ni kutokana na mashine zilizokuwa zikiyafyatua kukabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme, huku ujenzi huo ukijengwa na mafundi jamii.
Na Marco Maduhu - Malunde1 blog
TANZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Charles Kabeho akivunja matofali ambayo yametumika kujenga majengo matano katika kituo cha afya Kambarage mjini Shinyanga na kubaini yapo chini ya kiwango.Picha zote na Marco Maduhu na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Baadhi ya majengo ambayo yamejengewa matofali ambayo yamebainika kuwa chini ya kiwango.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Charles Kabeho akiendelea kukagua matofali katika kituo cha afya Kambarage.
Majengo yaliyodaiwa kujengwa na matofali mabovu.
Ukaguzi wa matofali ukiendelea.
Matofali yakiendelea kuvunjwa ambapo yalikuwa yakipukutika kama biskuti.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Charles Kabeho akiweka jiwe la msingi katika mradi wa maji kwenye kijiji cha Galamba Kata ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Charles Kabeho akikagua ujenzi wa matundu ya choo sita katika Shule ya msingi viwandani na kubaini kuwapo na dosari za ukamilishwaji wake huku Mhandisi wa manispaa hiyo Richard Makonobi akiukimbia mradi huo kwa kuogopa kutoa majibu ya ucheleweshwaji wake.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Charles Kabeho akiweka jiwe la msingi katika majengo ya kuishi walimu kwenye chuo cha Ualimu Shycom.
Awali Mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Taraba (kushoto) akimkabidhi mwenge wa uhuru mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko tayari kwa kuukimbiza manispaa ya Shinyanga ambapo umekimbia kilomita 63,5 kwa kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi Sita yenye thamani ya Shilingi Bilioni 18.46.
Mwenge wa uhuru ukiwa unakimbizwa katikati ya mji wa Shinyanga.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI WAKATI MWENGE WA UHURU UKIWA KATIKA VIWANJA VYA SABASABA KAMBARAGE MJINI SHINYANGA
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mhandisi Charles Kabeho akitoa ujumbe wa Mwenge mwaka 2018 katika viwanja vya Sabasaba Kambarage Mjini Shinyanga
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mhandisi Charles Kabeho akizungumza na wananchi
Katibu tawala wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi akisoma taarifa ya wilaya kwa kiongozi wa mbio za mwenge
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akitambulisha viongozi mbalimbali
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Abuu Gulam akijitambulisha
Katibu tawala mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akijitambulisha
Picha zote na Marco Maduhu na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Post A Comment: