IKIWA ni muda mfupi baada ya akaunti za Instagram yenye jina la Chadema_in_blood kuchapisha taarifa kwamba Mbunge wa Chalinze (CCM) ambaye pia ni mtoto wa Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete, Ridhiwani Kikwete amekishutumu chama chake kwa kukubali kupokea wapinzani wanaohamia kwenye chama hicho, mbunge huyo ameibuka na kukanusha taarifa hizo.
Akifafanua kuhusu uzushi huo, Ridhiwani amesema hajawahi kusema wala kuandika maneno hayo, yanayolenga kukiambia Chama na Serikali yake, hivyo ujumbe huo upuuzwe mara moja.Aidha, amesema hatokuwa tayari kusema neno ambalo litapotosha kiapo chake kama Mwanasheria ninayeheshimu Haki na Usawa katika Binadamu.
Ujumbe huo ulisomeka hivi;
“Ridhiwani MTOTO WA KIKWETE AITOLEA UVIVU SERIKALI YA CCM NA CHAMA CHAKE.
“Amjuza yakuwa Serikali yetu isipobadilika miaka yake (5) mitano itaisha kwa kufanya Uchaguzi kila mwezi wa marudio kila kuitwapo leo limegeuka kuwa Big Deal kwa CCM kwa minajili ya kufanya Spining.
“#Ashangaa serikali haijishitukii kumaliza fedha za wananchi kila kukicha kwenye chaguzi baada ya kuzitumia kwenye mahitaji ya wananchi ili kuwaletea maendeleo.
“Wakati wananchi hawana uhuru kupata habari za Bunge live kwa kisingizio cha kubana matumizi, leo gharama za kuendeshea, uchaguzi wa marudio Kinondoni peke yake unaigharimu serikali 1 bn Tsh.
“Hata kama wabunge na madiwani wa upinzani wanakipenda sana chama chetu na wanatamani sana kumuunga mkono Mhe Rais John Pombe Magufuli, hebu tusiwapokee, tuwaambie “Kaeni huko mtahamia 2020” ili fedha hizi tuzipeleke kwenye miradi ya maji, umeme, na elimu.
“Leo hii wananchi wangu wa Chalinze hawajui ni lini dawa zitaletwa kwenye Zahanati, Vituo vyao vya Afya na Hospital za Rufaa, lakini Kila kukicha ni habari ni chaguzi za marudio.
“Hebu CCM tujitathmini sana na huu muda tunaoupoteza kila mwezi kufanya chaguzi za marudio, wananchi wana akili wanayaona haya. Tusipobadilika sasa 2020 watatuhukumu.
Ridhiwani Kikwete.”
Ridhiwani Kikwete akajibu;
“Ikumbukwe Ndg. Watanzania wenzangu na Ususani WanaCCM wenzangu, Mapema Mwanzoni mwa Mwaka huu 2018,Tarehe 22 Niliutaarifu Umma Ukweli juu ya kile Nilichokiita Maneno ya Kiuchonganisha yanayolenga kunigombanisha Mimi na Uongozi wa Chama Changu CCM.
“Kupitia Ujumbe mdogo huo wa Video Nilikanusha juu ya maneno hayo kwamba Sikuyaandika mimi na wala Sina Uhusiano wowote na Maneno hayo. Lakini la kushangaza Baada ya Miezi Saba, jambo hilo linaibuka tena leo. Nimeweka video niliyoirusha Tarehe 22 January Usiku huo Nikielezea kutofurahishwa kwangu na kitendo hicho kilichofanyika.
“Sijawahi sema wala kuandika maneno hayo, yanayolenga kukiambia Chama na Serikali yangu kupuuza hawa Wanaohamia Chama na Kupelekea kufanyika Chaguzi za Mara kwa Mara. Nataka kuwahakikishia, kama Mwanasheria ninatambua Haki aliyonayo Raia Kikatiba. Sintokuwa tayari kusema neno ambalo litapotosha Kiapo Changu kama Mwanasheria ninayeheshimu Haki na Usawa katika Binadamu.
“Ndugu Watanzania wenzangu napenda kuwahakikishia kuwa Sihusiki na Maneno hayo na Ninawaomba sana muyapuuze.
Mimi
Ridhiwani Kikwete (Mb).”
Post A Comment: