Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ameitisha kikao na wakurugenzi wa manispaa zote za mkoa kwalengo la kupitia takwimu za mapato na matumizi ya mkoa huo ili kujiridhisha kwanini wameshuka kimapato na kuzidiwa na jiji la Dodoma ambalo limepandishwa hadhi hivi karibuni.
Makonda ametoa kauli hiyo leo Agosti 3, 2018 katika hafla ya kuwakaribisha wakuu wa wilaya wapya na kuwaaga waliohamishwa vituo vya kazi, ambapo amemtaka katibu tawala wa mkoa kuipanga upya Idara ya Ardhi kwani ni maeneo yenye uongo mwingi na imekuwa na viongozi ambao wanachukuwa nyaraka za wananchi na kisha kuwapelekea matajiri na kuwanyima haki wanyonge.
“Haiingii akilini Mkoa wa Dar es Salaam kushuka kimapato pamoja na kuzidiwa ukusanyaji kodi wakati ni mkoa wa kiuchumi, kuna nyumba na viwanja vya serikali ambavyo vimechukuliwa na watu binafsi, mikataba ya unyonyaji ambayo imesainiwa na inaiminya serikali”, amesema
Makonda ameongeza kuwa viongozi wengi wa Dar es Salaam wanatoa taarifa nyingi za uongozi juu ya utendaji na utekekezaji wa miradi na mfumo wa biashara pia uangaliwe ili kuiwezesha kuwepo kwa mfumo rahisi ambao unarahisisha huduma za kitengo cha biashara kwani kumekuwa na urasimu uliopitiliza.
“Katika suala la ulinzi na usalama, wanaendelea na kuweka Camera katika maeneo mbalimbali ya jiji na baada ya hapo tutaruhusu ufanyaji wa biashara kwa masaa24”, ameongeza Makonda.
Agosti 1, 2018 wakati akizungumza na wakuu wa mikoa baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, Rais Magufuli alisema kati ya majiji yote, Dodoma inaongoza kwa makusanyo ya mapato ya Shilingi bilioni 24.2 ikiwa ni asilimia 123 ya makisio yao ya Shilingi bilioni 19.
Amesema Jiji la Dar es Salaam ambalo ni kongwe kuliko yote lilikusanya pesa kidogo tofauti na ukubwa wake ambapo lilikusanya kiasi cha Sh15.3 bilioni, Arusha (Sh10.3 bilioni), Mwanza (Sh9.3bilioni), Tanga (Sh9.1bilioni) na Mbeya (Sh4.2bilioni).
Post A Comment: