Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Profesa Faustin Kamuzora, amemtambulisha rasmi Mpigachapa MKuu mpya wa Serikali, Maximillian Masesa ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuchukua nafasi hiyo baada ya aliyekuwa Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo kustaafu kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa umma.
Mpigachapa Mkuu wa serikali mpya, Maximillian Masase awali alikuwa Mkuu wa Kiwanda cha Uchapaji cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Akizungumza na watumishi wa Idara ya Kupigachapa ya jijini Dar es salaam leo tarehe 16 Agosti, 2018, wakati akimtambulisha Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu, Profesa Kamuzora amemtaka Mpigachapa huyo kuharakisha kuanza kwa uendeshaji wa shughuli za Wakala ya Uchapaji ya Serikali (Tanzania Government Printing Agency – TGPA).
Profesa Kamuzora amefafanua kuwa Serikali imeamua na kuridhia kuipandisha hadhi iliyokuwa Idara ya Kupigachapa ya Serikali na Kuwa Wakala ya Uchapaji ya Serikali lengo likiwa ni kuchapisha nyaraka kwa ubora, ufanisi na tija zaidi ili kuongeza mapato ya Serikali.
Akiongea mara baada ya kutambulishwa kwa watumishi wa Idara ya Kupigachapa ya serikali, Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Bwana Maximillian Masesa amemuhakikishia Katibu Mkuu, Profesa Kamuzora kuwa atasimamia kwa weledi na ufansi katika kuharakisha kuanza kwa uendeshaji wa shughuli za Wakala ya Uchapaji ya Serikali.
Aidha; baadhi ya majukumu yatakayosimamiwa na Mpigachapa Mkuu wa Serikali huyo ni pamoja na Kusimamia Uchapaji wa Nyaraka zote za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Taasisi zake pamoja na kuwa Msimamizi na mchapishaji wa Nyaraka zote za Serikali ikiwemo Nembo ya Taifa na nyaraka za uchaguzi.
Majukumu mengine ambayo atayasimia kupitia Wakala hiyo ni Kuhifadhi nyaraka mbalimbali za Serikali ni Kudhibiti uchapaji wa nyaraka zote za Serikali na kuhifadhi Siri na usalama wa nyaraka hizo pia, kutoa ushauri kwa Serikali juu ya mabadiliko ya teknolojia ya uchapaji Kimataifa sanjari na matumizi na mifumo ya nyaraka za Serikali;
Idara ya Kupigachapa ya Serikali ilianzishwa mjini Tanga mwaka 1905 wakati wa Utawala wa Kijerumani na kuhamishiwa Dar es Salaam baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia amabapo Serikali ya Waingereza walipewa jukumu la kuisimamia Tanganyika. Mwaka 1961 baada ya uhuru wa Tanganyika idara hiyo ilirithiwa na serikali, kwa sasa idara hiyo inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Post A Comment: