Mkuu mpya wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo ameapishwa leo huku akipewa onyo kuepuka wapotoshaji. Pamoja na Jokate, Zainab Kawawa naye ameapishwa kuwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo.

Jokate, ambaye aliwahi kuwa mlimbwende wa mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2006, aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Julai 28 mwaka huu.

Jokate ameapishwa leo Agosti 3 huku ndugu, jamaa, marafiki na viongozi wa CCM wakihudhuria hafla za uapisho huo.

Akizungumza mara baada ya wakuu hao wawili wa wilaya kuapishwa, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani, Ramadhani Maneno amewataka wateule hao waepuke wanaofika ofisini kutaka kuwapotosha katika utendaji wao.

Amewataka wakakae na makatibu tawala ili wakusanye mapato kwani mkoa wa Pwani una  viwanda.

“Kwa nafasi mlizopata hakikisheni mnakua karibu na viongozi wa chama hilo ni jambo kubwa. Wakati sasa mnaenda kuripoti kwenye wilaya mkaanzie kwenye ofisi za chama,”amesema.

Ameongeza: "Huko mnapoenda mtafute desturi na mila za maeneo yenu msizipuuzie, lakini mtafute yale yanayoendana na nyaraka zilizopo.”

Amesema anawakabidhi vitu vitatu, macho, masikio na mdomo ambavyo vitawasaidia kwenye utendaji wao wa kazi.

Pamoja na kuwepo kwa idadi ndogo ya waliohudhuria sherehe hizo za uapisho, hakuna msanii hata mmoja aliyeonekana.

Wengi walitarajia kuona wasanii wakijitokeza kwa wingi katika sherehe hizo kwa kuwa Jokate ni msanii wa filamu, muziki na ni mwanamitindo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: