Mkuu Wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza kiwango cha ukusanyaji mapato katika halmashauri hiyo.

Muro ameyasema hayo  jana Jumamosi Agosti 11, katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na kuongeza kuwa vipo vyanzo vingi vya mapato ambayo halmashauri hiyo inaweza kukusanya hadi kufikia Sh bilioni 10.

Amesema itafika mahala watashindwa kugharamia vikao vyao, mtashindwa kupata posho kwa sababu hatakuwa tayari kutoa fedha badala ya kwenda kulipa malimbikizo ya madeni ya walimu wakati wao hawatimizi wajibu wao.

“Hilo katika uongozi wangu mtalisahau, twendeni kwa pamoja tuwasimamie wale, tupambane, tuongeze mapato ya kutosha hata mkilipana posho wananchi hawatatuona sisi wezi, tutasema tumelipa posho diwani ambaye anazunguka katika maeneo yake anakagua na kusimamia maofisa tarafa na watendaji katika kata yake.

“Lakini wako madiwani hawajawahi hata kumsalimia sekretari wake asubuhi akiamka hamuulizi hata Ofisa Mtendaji wake, umeamkaje, kuna nini kipya, unaendeleaje umefuatilia ule mradi.

“Iko miradi ya serikali mikubwa, mmeweka kwenye taarifa hapa, kuna ofisa mtendaji hajui wajibu kwenye ule mradi ni kwenda kukagua nondo, kiwango cha saruji kinachochanganywa, vifaa vinavyoletwa na maabara na vitu kama hivyo,” amesema Muro.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Dk. Wilson Mahera amesema iko baadhi ya miradi iliyokamilika na inatarajiwa kuzinduliwa na mbio za mwenge wa uhuru wilayani humo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: