Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akisisitiza jambo kwa Wakuu wa Wilaya wapya 27 walioteuliwa hivi karibuni katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Taifa ya ukaguzi, Jijini Dodoma leo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe akisisitiza umuhimu wa kufuata sheria , taratibu na kanuni katika utekelezaji wa majukumu katika Kikao kazi cha Wakuu wa Wilaya wapya walioteuliwa hivi karibuni kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya wapya wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (hayupo pichani) katika Kikao kazi cha Wakuu wa Wilaya wapya walioteuliwa hivi karibuni kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Jijini Dodoma
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya wapya wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (hayupo pichani) katika Kikao kazi cha Wakuu wa Wilaya wapya walioteuliwa hivi karibuni kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Jijini Dodoma
Zulfa Mfinanga.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amewataka Wakuu wapya wa Wilaya walioteuliwa hivi karibuni kuhakikisha wanasoma na kuzielewa sheria zinazowaongoza ili kufanya kazi kwa weledi.
Mhe. Jafo aliyasema hayo leo Jijini Dodoma kwenye kikao kazi na Wakuu hao wa wilaya kwa lengo la kuwapa maelekezo ya kazi ambapo aliwaambia mada kuu ya kikao hicho ni mahusiano na mawasiliano kazini pamoja na kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
“Msiende kuwa vyanzo vya migogoro kwenye Wilaya zenu, tumekuwa tukishuhudia migogoro baina ya Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Wenyeviti wa Halmashauri, Makatibu Tawala pamoja na Wabunge, hatuwezi kwenda hivi, katengenezeni serikali” Alisema Waziri Jafo.
Hata hivyo alikemea tabia ya baadhi ya Wakuu wa Wilaya kuitumia vibaya mamlaka waliyonayo na kuwaweka watu ndani hali iliyopelekea wananchi kuichukia serikali yao, hivyo kuwataka kutumia sheria kama iliyokusudiwa na siyo kwa kuonea watu.
Aidha aliwataka Wakuu hao wapya wa Wilaya kutoa ushirikiano kwa wale wanaotekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na siyo vinginevyo ikiwa ni pamoja kusimamia miradi ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya afya na elimu unaoendelea kote nchini.
Kwa upande mwingine Waziri Jafo amesema “Kasimamieni ukusanyaji wa mapato ya serikali kupitia mfumo wa kieletroniki sambamba na kudhibiti uvujaji wa mapato hayo, lakini pia mkadhibiti madeni kwa kuwa fedha hizo ndizo zinazotegemewa kwa ajili ya maendeleo nchini”.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Injinia Mussa Iyombe amewataka Wakuu hao wa wilaya kuzitendea haki nafasi walizopewa kwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo hasa pale wanapomuadhibu mtumishi aliyekosea.
“Serikali ina taratibu zake, baadhi ya wakuu wa wilaya walikuwa wanatia aibu, kama kuna mtumishi kakosea, tumia mamlaka zinazomuongoza kumshughulikia, na sio kusimamisha watu kazi hovyo, kutumbua tumbua hovyo” Alisisitiza Injinia Iyombe.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro kwa niaba ya wakuu wenzake wa wilaya amesema watahakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.
Post A Comment: