Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania kuendelea kusimamia maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kuhakikisha hayajihusishi na utakasishaji fedha haramu.
Alitoa agizo hilo wakati alipofanya mazungumzo na Gavana wa Benki Kuu, Prof. Florens Luoga na Manaibu Gavana, Bw. Julian Banzi Raphael, Dkt. Bernard Kibesse na Dkt. Yamungu Kayandabila Ikulu, Zanzibar tarehe 28 Agosti, 2018 walipokwenda kujitambulisha.
Dkt. Shein alisema kwa siku za karibuni, maduka hayo yamekuwa yakituhumiwa kujihusisha na utakasishaji wa fedha haramu, na amenesha kukerwa na matumizi makubwa ya fedha za kigeni (dollarization) hapa nchini na kuagiza suala hilo lishughulikiwe haraka.
“Haiwezekani tunapoenda Uingereza tulipe paundi na nchini mwetu pia watutake kulipa kwa paundi ya Mwingereza,” alisema Rais.
Rais huyo aliwasifu Gavana na wasaidizi wake kwa kusimamia ipasavyo masuala ya uchumi, hali inayochangia uchumi kukua vizuri.
“Si kazi rahisi kusimamia masuala haya ya uchumi kwani wenzetu wa nchi zilizoendelea wameanza siku nyingi sana, hatuwezi kujilinganisha nao,” Rais alisema.
Mapema katika maelezo yake, Gavana Luoga alieleza kwamba lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kujitambulisha kwa Mhe. Rais na kufanya mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali ya Benki Kuu na sekta ya fedha kwa ujumla.
Prof Luoga alimfahamisha Mhe. Rais kuwa Benki Kuu inaendelea kuwa imara katika kutekeleza majukumu yake ya msingi na kwamba viashiria vyote vinaonyesha kuwa Taasisi iko vizuri.
Mathalani, kuhusu jukumu la msingi la Benki Kuu ambalo ni kuhakikisha kuna utulivu wa bei, kiashiria chake ni mfumuko wa bei, eneo ambalo hali nzuri, kwani lengo ni kuwa na mfumuko wa bei usiozidi asilimia 5. Akizungumzia sekta ya mabenki, Prof Luoga alisema; “pamoja na changamoto zake, hususan, uwepo wa mikopo chechefu, bado sekta hii ni thabiti na inasimamiwa vizuri. Benki Kuu imeshachukua hatua kadhaa za kudhibiti hali hii na inafuatilia kwa karibu kuhakikisha kuwa tunaondokana na tatizo hili la mikopo chechefu.”
Akizungumzia akiba ya taifa ya fedha za kigeni, Gavana alisema hali ni ya kuridhisha, kwani tuna akiba ya kutosha uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje za kukidhi kipindi cha miezi mitano.
“Aidha, mahusiano yetu na serikali ni mazuri sana kwa sababu tunaamini sera za kibajeti na sera za fedha ni vyema zisemezane”, aliongeza Gavana. Prof Luoga alimhakikishia Mhe. Rais kuwa yeye na viongozi wenzake wataendelea kuisimamia Benki Kuu kwa uadilifu na kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Akimjibu Prof Luoga, Mhe. Rais wa Zanzibar alianza kwa kuwashukuru viongozi hao kwa kumtembelea kwa ajili ya kufahamiana, na pia kubadilishana mawazo. Pia, alimshukuru Prof Luoga kwa kukubali uteuzi wa nafasi ya Gavana kwani angeweza kukataa.
Dkt. Shein alisema anafarijika sana kuona kuwa Benki Kuu ya Tanzania iko imara na inazidi kutekeleza majukumu yake vizuri. “Nikiangalia tu nyuso zenu nawaona kabisa kuwa ninyi ni watu makini mtakaoisimamia vema sekta ya fedha, hivyo imani yangu kwenu ni kubwa sana,”alisema Mhe. Rais.Pamoja na viongozi hao wakuu wa Benki Kuu, ujumbe wa BoT uliwashirikisha Kaimu Mkurugenzi wa Tawi la BoT Zanzibar, Ndugu Suleiman Masudi, Msaidizi wa Gavana Dkt Nguling’wa Balele na Meneja Uhusiano wa Umma na Itifaki, Bibi Zalia Mbeo.
Post A Comment: