Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi Joseph Mkirikiti amemkabidhi na kumuomba mkuu mpya wa wilaya hiyo Hashim Mgandilwa, kutekeleza majukumu yake bila kuogopa na kuwa hakuna kisichowezekana kutekelezwa kama ataweka nia katika kuyafikia malengo aliyojiwekea katika kuwahudumia wananchi.
Akiongea leo wakati wa makabidhiano ya ofisi hiyo Mkirikiti amesema kwa nafasi yake aliweza kutekeleza majukumu yake katika kipindi chote cha miaka miwili alichohudumu nafasi hiyo ya ukuu wa wilaya hiyo.
"Yapo ambayo niliyaweza na yapo mengine labda kibinadamu niliyashindwa, lakini yote kwa yote nilijitahidi kutimiza wajibu wangu kama unavostahili kwa nafasi ya mkuu wa wilaya" Alisema Mkirikiti.
Aidha kwa upande wa DC Hashim Mgandilwa ameshukuru kwa mapokezi mazuri huku akiwaomba viongozi wa ulinzi na usalama na watendaji wengine kumpa ushirikiano wa hali na mali katika kuhakikisha wanasukuma gurudumu la maendeleo kwa ajili ya watu wa Ruangwa.
Aidha Mgandilwa ameahidi kutembelea vijiji vyote vya wilaya hiyo ili kufanya utambuzi na kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
"Sisi tuliopo hapa ndio watu ambao tumepewa dhamana kwa niaba ya wao, kwenye ofisi ambazo tumekuja kila mmoja kuna changamoto, si wakati wa kulia na kuzisema changamoto badala yake ni kuhakikisha hizi changamoto tulizonazo zinatatulika". alisema Mgandilwa.
Post A Comment: