Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), kimetangaza majina ya wagombea wake watakaowania ubunge katika majimbo ya Ukonga, Korogwe Vijijini na Monduli kupitia kikao cha kamati kuu ya chama.

Katibu wa chama hicho kanda ya kaskazini Amani Golugwa ameiambia tovuti ya www.eatv.tv kuwa tayari chama hicho kupitia mkutano wake kimekwisha pitisha majina ya watakaopeperusha bendera za chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Septemba 16, 2018.

Golugwa amewataja wagombea hao kuwa ni Amina Ally atakayegombea ubunge jimbo la Korogwe Vijijini, aliyekuwa Diwani wa kata ya Lepurko Yonas Masiaya Laizer atasimama jimbo la Monduli pamoja na Asia Msangi atakayeiwakilisha Chadema jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo matatu na wa udiwani katika kata mbili za Tanzania Bara utakaofanyika Septemba 16, mwaka huu.

“Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Ubunge katika majimbo matatu majimbo hayo kuwa ni Korogwe Vijijini, Mkoa wa Tanga kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Stephen Hilary Ngonyani, Jimbo la Ukonga katika mkoa wa Dar es Salaam na Jimbo la Monduli mkoani Arusha baada ya waliokuwa wabunge wa majimbo hayo kujiuzulu uanachama wa CHADEMA hivyo kukosa sifa za kusalia wabunge”, ilisema taarifa ya tume.

Uchaguzi huo utafanyika ikiwa ni mwezi mmoja kupita tangu ufanyike uchaguzi mwingine mdogo katika jimbo la Buyungu wilayani Kakonko mkoani Kigoma pamoja na kata 79 nchini ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kilishinda kwa asilimia 100%.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: