NAIBU Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu, amesema milango ipo wazi kwa wabunge na madiwani wa chama hicho wanaokubali kurubuniwa na kukikimbia chama.

Alisema wabunge na madiwani hao hawana dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi, hivyo wanaweza kwenda wanakorubuniwa.

Alisema hayo mwishoni mwa wiki mjini hapa wakati akiwahutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Bagara, Mathias Zebedayo.

"Kwa wale wenye njaa watakwenda, kwa wale wasio na hofu ya Mungu watakwenda na kwa wale ambao walikuwa hawana dhamira ya kweli watakwenda kwa kuwa walihitaji udiwani na ubunge, lakini wanaohitaji mapinduzi ya kweli watabaki,'' alisema.

Aidha, alidai Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilizoea kutumia nguvu za dola kuwaibia kura wapinzani wakaona mbinu hiyo haitoshi, sasa wameamua kuanza kuwanunua wabunge na madiwani.

Alisema Chadema inawaacha wabunge na madiwani wanaokubali kununuliwa ili waende kushirikiana na watu waliozoea wizi na ufisadi katika majimbo yao na halmashauri zao na kusababisha huduma za kijamii kukosekana.

Aliwaomba wakazi hao kumchagua mgombea udiwani wa Chadema ili waendelee kuleta maendeleo katika halmashauri hiyo kwa kuwa wameshaonyesha njia.

Alisema kwa mfano, wakati wanaichukua halmashauri walikuta makusanyo kwa mwezi ni Sh. milioni 700, lakini kwa sasa halmashauri chini ya Chadema inakusanya Shilingi bilioni mbili ambazo zinasaidia kuwaletea maendeleo.

Akizungumza Nipashe baada ya mkutano huo kuhusu namna walivyojipanga kudhibiti wimbi la wabunge na madiwani kuhamia CCM, alisema, hawana mpango wowote kudhibiti wimbi hilo kwa kuwa wabunge hao na madiwani ni watu wazima na walijiunga na chama kwa hiari yao.

Akimwombea kura za ndiyo mgombea wa Chadema, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul, aliwataka wananchi kujipanga kulinda kura zao.

"Wale ambao wamezoea kutuonea kwenye uchaguzi na kutuibia kura zetu awamu hii tumeandaa wazee wa kimila, ili wakituhujumu kwa njia yoyote wafe mtaona watakavyolaliana hapa wakifa mmoja baada ya mwingine,'' alisema.

Mgombea udiwani wa Kata ya Bagara, Mathias Zebedayo, aliwaomba kumchagua ili aweze kuyaendeleza yale yote aliyoshindwa mtangulizi wake kwa miaka mitatu iliyopita na kutimkia CCM.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: