Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amemweka ndani Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Mtwara (OCS), Ibrahim Mhando kwa kushindwa kuwaweka mahabusu watuhumiwa wanne.
A
Miongoni mwa watuhumiwa hao ni mhandisi mshauri wa kampuni ya Y&P Architects, Benjamin Kasiga ambaye anadaiwa kutoa taarifa ya uongo kwa waziri huyo kuhusu ujenzi wa ofisi ya Uhamiaji mkoani humo.
Tukio hilo limetokea leo asubuhi Agosti 27, 2018 wakati Lugola na katibu mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu walipofika katika kituo hicho kwa kushtukiza.
Lugola alipokuwa anakwenda uwanja wa ndege kwa ajili ya kurudi jijini Dar es Salaam, alitaka kuthibitisha kama mtuhumiwa ambaye alielekeza jana usiku akamatwe awekwe mahabusu kama polisi walitekeleza agizo lake.
Hata hivyo, Lugola alimkuta mtuhumiwa huyo akiwa chumba cha upelelezi badala ya kuwekwa mahabusu ya polisi, hivyo akamuuliza kamanda wa polisi wa mkoa huo, Lucas Mkondya sababu za kutotekelezwa agizo lake.
“Hivi ndivyo polisi mnafanya hivi, haya ndiyo madudu mnayoyafanya? Tabia hii siku zote tunaipinga ikichafua Polisi na hii ndiyo tabia yenu. Najua ndiyo mana nimekuja ghafla, mnafahamu maadili ya Jeshi,” alihoji Lugola.
“RPC hawa polisi wako wanafanya nini? OCS njoo hapa, kwa nini umeweka hawa watuhumiwa chumba cha upepelezi badala ya mahabusu, nawe unaingia ndani kwa kushindwa kuwaweka ndani hawa watuhumiwa, RPC muweke ndani sasa hivi huyu,” aliamuru Lugola.
Hata hivyo, Mkondya alimweleza Lugola kuwa polisi wake walifanya makosa kwa kutowaweka mahabusu watuhumiwa hao.
Naye mkuu wa kituo hicho, Mhando kabla ya kuwekwa mahabusu pamoja na wale watuhumiwa ambao alishindwa kuwaweka mahabusu, amesema sababu kubwa ya kutowaweka mahabusu ni kwamba chumba kilijaa na wanafanya hivyo mara chache inapotokea.
Lugola aliipinga kauli hiyo kuhusu mahabusu hiyo kujaa wakati nafasi ya kukaa watuhumiwa hao ilikuwapo ndani ya mahabusu hiyo.
“Mbona nafasi ipo pale mahabusu, ile pale nafasi naiona, siwezi kukubaliana na uzembe huu na hii ni tabia yenu huwa mnakamata watuhumiwa lakini baadhi hamuwaweki mahabusu, unanidanganya kuwa mahabusu imejaa, hii haikubaliki!” amesema Lugola.
Post A Comment: