Winfrida Emmanuel (18) mkazi wa kijiji cha Mwagala, Kata ya Ukiriguru wilayani ya Misungwi jijini Mwanza amejifungua watoto pacha kwenye beseni akiwa wodi ya wazazi katika hospitali ya wilaya baada ya kukosa huduma.

Tukio hilo limetokea jana Agosti 27,2018 saa 1:00 asubuhi hospitalini hapo.

Akizungumza na Mwananchi hospitalini hapo mama mzazi wa Winfrida, Flora Lugwisha amesema alimfikisha mwanaye katika hospitali hiyo saa 9:00 usiku baada ya kupewa rufaa kutoka zahanati ya kijiji cha Mwagala.

“Tulifikia mapokezi na usiku huo tulianza kusumbuliwa na wauguzi mara nendeni wodini, tulipofika wodini nikawaeleza nesi tatizo la mtoto wangu anaumwa tumbo chini ya kitovu, akaniambia ana kazi, nikampeleka kitandani mtoto alianza kulalamika uchungu wakati huo tayari saa 12:00 asubuhi,” amesema.

“Nilirudi kwa nesi, akanieleza ana kazi na kunielekeza kwenda wodi ya watoto nikamtafute nesi mwingine lakini niliwakosa, nikarudi mtoto akanieleza anataka kujisaidia haja kubwa nikamweleza nesi akasema unanisumbua nikampelekea beseni wakati anataka kujisaidia akatoka mtoto wa kwanza baadaye akatoka mwingine saa 1:10 asubuhi,” ameongeza.

Katika maelezo ya Flora anasema watu waliokuwamo wodini walianza kulalamika na miongoni mwao walitokea wanawake sita wakambeba mmoja akabeba beseni na kumpeleka chumba cha kujifungulia.

“Nesi alipoona hivyo ndipo alishtuka akaanza kuniomba wembe nikamwambia sina lakini badaye wembe ulipatikana akaanza kuwakatia,” amesema Flora.

Mary Bujukano ni mmoja wa mashuhuda waliotoa msaada wa kumbeba mzazi ambapo amesema “mama yake (Winfrida) alipata taabu sana kutafuta huduma na kujikuta mzazi anajifungulia kwenye beseni. Kweli tulimsaidia kumbeba na kumpeleka chumba cha kujifungulia wakati tayari amejifungua watoto pacha.”

Kabula Malemi mkazi wa kijiji cha Mwambola ambaye naye amempeleka mjamzito hospitalini hapo amesema huduma zao zinasikitisha kwani manesi hawahudumii wagonjwa kama inavyotakiwa.

Kwa upande wake, mganga mkuu wa hospitali ya wilaya hiyo, Dk Zabron Masatu amethibitisha kuwapo tukio hilo huku akidai kuwa wakati tukio linatokea wodi ya wazazi alikuwapo muuguzi mmoja na kwamba aliposikia kelele aliingia wodini akamkuta tayari amejifungua.

Hata hivyo, Dk Masatu amesema wanafanya uchunguzi zaidi na endapo ikithibitika ni uzembe wa muuguzi atachukuliwa hatua zaidi.

Kuhusu afya za pacha hao, Dk Masatu amesema pacha mmoja, Dotto amezaliwa utumbo wake ukiwa nje hivyo wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando.


Na Twalad Salum, Mwananchi
Share To:

Anonymous

Post A Comment: