Na Mathias Canal-WK, Bukoba-Kagera
Malalamiko ya muda mrefu ya wakulima yaliyokuwepo kwamba ushirika unatoa bei ndogo, sasa yamepatiwa muarobaini baada ya serikali kupitia kwa kina gharama za uendeshaji na uongezaji thamani kwa zao la kahawa kwa Vyama vikuu vya ushirika Mkoani Kagera.

Serikali imepiga marufuku kwa vyama hivyo vya ushirika kutoza zaidi ya shilingi 490 kwa kilo moja ya Kahawa ya maganda kama gharama za uendeshaji na uongezaji thamani, Awali maainisho ya gharama hizo yalikuwa ni makubwa ambapo kiasi cha shilingi 1350 kwa kilo moja ya Kahawa ya maganda ilianishwa kama gharama za uendeshaji.

Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba ameeleza agizo hilo jana 12 Julai 2018 wakati akizungumza na wajumbe wa Halmshauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera kwenye Hoteli ya Bukoba Coop ambapo miongoni mwa ajenda ya kikao hicho ilikuwa ni kujadili kuhusu soko la Kahawa na uendeshaji wa ushirika.

Dkt Tizeba amewaeleza wajumbe hao kuwa amepiga marufuku hiyo kufuatia malalamiko ya wadau wa Kahawa Mkoani Kagera ambapo gharama hizo zilionekana kuwa kubwa ukilinganisha na gharama halisi.

"Ndugu zangu wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM inawezekanaje shilingi mia mbili inatozwa kama ushuru wa chama kikuu, na shilingi mia mbili tena inatozwa kama ushuru wa chama cha msingi, ni nani anaweza kukupa faida namna hii sasa rasmi ushuru huu tumeupunguza kama nilivyoeleza" Alikaririwa Mhe Tizeba

Aliongeza kuwa swala la ushirika ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ni mkataba kati ya wananchi na serikali katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015-2020 kwa imani kubwa kwamba ndicho chombo pekee kitakacho mkwamua mkulima na changamoto anazo kabiliana nazo kwenye Kilimo na masoko ikiwa ni pamoja na kujiondoa katika umasikini.

Aidha, Dkt Tizeba aliwaeleza wajumbe hao kuwa vyama vya ushirika havipaswi kuendeleza mazoea ya kujiwekea gharama bila kwanza kutazama kipato cha mkulima huku akieleza kuwa amewaelekeza wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi ambapo Wilaya zao zinalima Kahawa kote nchini kufuatilia kwa karibu mwenendo wa masoko ya Kahawa kuanzia inavyokusanywa mpaka wakati inapouzwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera Bi Costansia Buhiye amempongeza Waziri huyo wa kilimo kwa kujibu kero namba 10 ya kikao cha Halmshauri kuu ya CCM kuhusu wasiwasi wa bei ya kahawa na namna na uendeshaji wa ushirika.

Buhiye alimpongeza Waziri huyo kwa kutatua kadhia mbalimbali za wakulima wa Kahawa katika ziara yake ya siku tatu Mkoani humo huku akieleza kuwa ana imani kubwa sasa kuwa wajumbe hao watatembea kifua mbele endapo wakulima wao watapatiwa bei nzuri.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: