WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka sheria kali zinazowalinda watoto wa kike na watakaobainika kuwapa ujauzito na kukatisha masomo yao adhabu watakayoipata hawatoisahau maisha.
Aliyasema hayo jana (Jumapili, Julai 29, 2018) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mwakizega wilaya ya Uvinza akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma.
Alisema Serikali itatoa adhabu kali kwa mtu atakayebainika kukatisha elimu ya mtoto wa kike iwe kwa kumuoa au kumpa ujauzo.
Alisema watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na waachwa waendelee na masomo yao kwani elimu ni haki yao ya msingi.
“Tukikukuta na mwanafuzni wa kike kwenye kona zisizoeleweka adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 30 gerezani, hivyo vijana kuweni makini,” alisisitiza.
Pia Waziri Mkuu aliwataka wazazi na walezi kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wa kike wanapelekwa shule na wanamaliza masomo yao.
Waziri Mkuu aliwaasa wanafunzi wote kusoma kwa bidii ili watimize ndoto zao na wasikubali kushawishika kwa kuwa watashindwa kufikia masomo yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI 30, 2018.
Post A Comment: