WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imejenga vituo vya afya 108 na inatarajia kujenga vingine 68 katika mwaka huu wa fedha.
Ametoa kauli hiyo jana asubuhi (Jumanne, Julai 17, 2018) wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye kituo cha afya cha Chela, kata ya Chela katika Halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
Ameipongeza kamati ya ujenzi ya kijiji pamoja na watumishi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri ujenzi na kupata majengo yenye viwango kupitia "Force Account." Baadhi ya Halmashauri hutumia njia ya manunuzi ya “Force Account” badala ya kutumia wakandarasi ili kupunguza gharama na kukamilisha mradi ndani ya muda mfupi.
"Majengo haya yamegharimu sh. milioni 400, hongera wananchi na kamati ya ujenzi iliyosimamia hapa. Tumepata majengo mazuri kwa sababu ile kamati na watumishi wa Halmashauri ni waaminifu, ndiyo maana majengo yanapendeza," amesema.
Waziri Mkuu alise kuna ombi la zahanati lilitolewa na mmoja wa wabunge wa viti maalum wa mkoa huo lakini akatumia fursa hiyo kuwapa mwongozo wananchi kwamba ujenzi wa maboma ya zahanati hivi sasa unafanywa na wananchi na Halmashauri inamalizia kwa kutoa vifaa vya kuezekea.
"Tuna vijiji zaidi ya 16,000 kwa nchi nzima na tumesisitiza kila kijiji kiwe na zahanati. Tumeamua wananchi wajitolee kujenga boma na Halmashauri itamalizia kwa kutoa vifaa vya kiwandani kama mabati na misumari."
Alisema wanahitaji kujenga nyumba ya vyumba vinne ili wapate chumba cha mganga, chumba cha kufunga vidonda, cha sindano na cha kutolea dawa.
"Serikali yenyewe inaenda kwenye kata na kujenga vituo vya afya vyenye uwezo wa kutoa huduma zote ili wananchi wasipate taabu ya kusafiri hadi makao makuu ya wilaya," alisema.
"Kila kituo cha afya kinapaswa kiwe na maabara, chumba cha daktari, cha upasuaji, chumba cha kujifungulia akinamama wajawazito na chumba cha kupumzikia mama na mtoto. Pia kuwe na chumba cha sindano, vidonda na kutolea dawa," alisema.
Alisema vituo vyote vya afya vilivyojengwa vimepatiwa sh. milioni 500 kila kimoja za kununulia vifaa na samani.
Amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Bw. Simon Berege apeleke maombi kwenye Baraza la Madiwani ili waweze kuongeza majengo mawili, moja likiwa ni wodi ya akinamama na watoto ya magonjwa mchanganyiko na nyingine iwe ya akinababa ya magonjwa mchanganyiko.
Mapema, mbunge wa Jimbo la Msalala, Bw. Ezekiel Maige alisema wananchi wa kata hiyo wanakabiliwa na ukosefu wa soko la dengu, hali iliyosababisha bei ishuke sana.
"Wananchi wa kata ya Chela ni wazalishaji wakubwa wa dengu na msimu ukiwa mzuri, bei ya gunia moja inafikia sh. 200,000. Lakini sasa hivi, imeshuka hadi chini ya sh. 100,000. Tunaomba watafutiwe soko ili uchumi wa hapa uinuke," alisema.
Akiwa Chela, Waziri Mkuu alimtambulisha Mkuu mpya wa Wilaya ya Kahama, Bw. Anamringi Macha ambaye ameanza kazi leo hii baada ya kuapishwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bibi Zainab Tellack.
"Nimtambulishe kwenu Mkuu mpya wa Wilaya ya Kahama ambaye hajafikisha hata saa mbili tangu alipoapishwa asubuhi hii. Tayari ameanza kazi, na hii ndiyo Serikali ya Hapa Kazi Tu," alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Post A Comment: