Na Asteria Muhozya, Afisa Habari,Wizara ya Madini.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema anatamani kuona ifikapo mwezi Disemba mwaka huu, Serikali kupitia Wizara ya Madini inaanzisha Soko Huria la Madini nchini (Tanzania Mineral Exchange).

Waziri Kairuki aliyasema hayo tarehe 24 Julai, 2018, wakati wa kikao cha Menejementi ya Wizara ya Madini na Taasisi zake ambapo Wataalam kutoka Kampuni ya Tanzania Mecantile Exchange PLC  (TMC) waliwasilisha mada juu ya Elimu ya Soko la Bidhaa Tanzania.

Aidha, Waziri Kairuki aliishukuru kampuni hiyo kwa kutoa wasilisho hilo ikiwemo utaalam wao katika masuala ya soko huria la madini na kuongeza kuwa, anatamani kuona suala hilo linafanikiwa na kufanyika mapema kwa kuwa, litawezesha Watanzania kumiliki uchumi wa madini hata wale wenye kipato cha chini.

“Natamani kuona ndani ya kipindi cha miezi sita vinavyowezekana kufanyika vinaanza kufanyika. Lakini tutazingatia sheria, taratibu na utalaam kuhakikisha kwamba suala hili linafanikiwa,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Akiwasilisha mada, Mtaalam mwelekezi kutoka kampuni hiyo, Girish Raipurie, alieleza faida za soko huria la madini kwa Tanzania, huku akisisitiza kuhusu umuhimu wa kutolewa mafunzo kwa wadau na elimu ya kutosha kuhusiana na   suala hilo.

Pia, alieleza kuhusu namna ambavyo Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo zinafanya vizuri katika suala hilo huku akielezea mazingira wezeshi ambayo yanawezesha Tanzania kufanikiwa katika uanzishaji wa soko hilo, huku akijaribu kufananisha na mazingira ya nchini India ambayo mfumo wa soko hilo unafanya vizuri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMC, Godfrey Marekano, alitoa mada kuhusu Mpango wa uwekezaji katika Soko huria na pia amegusia kuhusu masuala ya kisheria na namna ambavyo Sheria ya Madini kama ilivyorekebishwa Mwaka 2017 inavyoweza kusimamia uanzishaji wa suala husika.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, alimpongeza Waziri Kairuki kwa kuanzisha wazo hilo ambalo litawezesha kuleta mageuzi katika Sekta ya Madini na kuwataka wataalam katika Wizara ya Madini na Tume ya Madini kulichukulia suala hilo kwa uzito ili utekelezaji wake uweze kufanyika kama ilivyopangwa.

“Kuna maelekezo mengi kwenye Sheria ambayo tunahitaji kuvipitia na kuyafanyia kazi. Maarifa tuliyoyapata ni makubwa. Rai yangu ni kwa wataalam kuhakikisha wanalichukulia suala hili kwa uzito mkubwa lisibaki mikononi mwa Waziri tu, alisisitiza Biteko”.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: