Wanafunzi wawili wa tumbo moja, Dotto Juma (10), aliyekuwa anasoma darasa la nne katika shule ya msingi Serengeti wilayani Bunda na Maduhu Juma (7) aliyekuwa anasoma darasa la awali shuleni hapo, wamekufa maji mtoni.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Serengeti, Marwa Samu, watoto hao walikufa maji baada ya kuogelea katika mto mkubwa ulioko katika eneo hilo na ndipo walipozidiwa na maji na kupoteza maisha.

Samo alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 10:00 jioni wakati watoto hao wakiwa wanachunga ng’ombe katika eneo hilo.

Kaka mkubwa wa marehemu hao, Kija James, alisema taarifa ya vifo hivyo ilitolewa na mtoto mwenzao, Kulwa Juma (10) waliyekuwa naye wakichunga mifugo hiyo.

James alisema baada ya kufika katika eneo hilo, walikuta nguo za watoto hao pembezoni mwa mto na walipomuuliza Kulwa, alisema walikuwa katika eneo hilo.

“Tulifika katika eneo hilo, ambako ni lile lile ulikokutwa mwili wa tajiri wa mabasi, Super Sammy. Tulipomuuliza Kulwa kwamba wenzake walikuwa wapi, alitujibu kuwa walikuwa katika eneo hilo,” alisema.

“Tulimuuliza kwamba huenda wamekwenda kuchungia ng’ombe sehemu nyingine akatujibu kwamba walikuwa hapo hapo tu,” aliongeza James.

Alisema juhudi za kuopoa miili yao zilifanyika na ndipo wazamiaji walipoingia ndani ya mto huo na kufanikiwa kuiopoa na kutoa taarifa polisi.

Ofisa mmoja wa polisi wilayani hapa, ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa madai kuwa si msemaji wa polisi, alisema miili ya marehemu hao ilihifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda na kwamba tayari imefanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: