Wahasibu watatu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za uhujumu uchumi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 50 ya mwaka 2018  niMercy Semwenda (49) maarufu Mercy  Frank Lema  mkazi wa Mwananyamala,Frola Bwahawa (54) mkazi wa Mbagala naHawa Tabuyanjaa (54) mkazi  wa Mwenge.

Jana Alhamisi Julai 12, 2018 wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita alidai mbele ya hakimu mkazi, Augustine Rwizile  kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya wizi na  kuisababishia hasara Serikali ya Sh 57.7milioni.

Katika shtaka la kwanza la wizi linalomkabili Mercy  pekee anadaiwa katika tarehe tofauti  kati ya Januari  Mosi,  Septemba 21, 2017 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa aliiba vocha za muda wa maongozi zenye thamani ya Sh44milioni.

Pia, anadaiwa kuiba fedha za mauzo kiasi cha Sh5.9milioni na fedha taslimu Sh 8.5milioni, vyote vikiwa na thamani ya Sh 57.7milioni mali ya TTCL, wakati akijua kuwa ni mtumishi wa shirika hilo.

Katika shtaka pili la kuisababishia Serikali hasara linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa katika kipindi hicho jijini Dar es Salaam, washtakiwa kwa makusudi waliisababishia TTCL hasara ya Sh57.7milioni.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, hakimu Rwezile alisema  washtakiwa hawatakiwi kusema chochote mahakamani hapo, kutokana na mashtaka yanayowakabili kuwa ni ya uhujumu uchumi.

Hata hivyo, Mwita alidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Wakili anayemtetea mshtakiwa wa pili na wa tatu, Thimotheo Wandiba alidai kuwa wanafanya utaratibu wa kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 24, 2018 itakapotajwa tena huku washtakiwa wakirejeshwa rumande.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: