Vikundi vinavyojihusisha na uzalisha mdogo vilivyopo kata ya Kawekamo wilaya ya Ilemela vimetakiwa kuunga mkono sera ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli ya kuwa na nchi yenye  uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha vinakuwa na uzalishaji wenye tija na ufanisi.

Kauli hiyo imetolewa na Diwani wa kata ya Kawekamo Mhe Japhes Rwehumbiza wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa kikundi cha Tupendane kilichopo ndani ya kata hiyo ambapo amevitaka vikundi vyote kuhakikisha vinaenda sambamba na malengo ya serikali kwa kuacha kufikiria kufa na kuzikana badala yake vijikite katika uzalishaji wenye tija na ufanisi unaoenda sambamba na sera ya nchi ya kuwa na uchumi wa kati kupitia uchumi viwanda

‘… Nadhani umefika wakati sasa tuache kufikiria kufa na kuzikana maana kila mtu amezaliwa lazima atakufa tu, Ninachowaomba ndugu zangu tuanze kuunga mkono sera ya srikali yetu ya kuwa na nchi ya uchumi wa kati kupitia viwanda vyetu …’ Alisema

Aidha Mhe Japhes amekemea vitendo vya baadhi ya viongozi  wa vikundi hivyo kutumia madaraka yao vibaya vya kuwabagua baadhi ya wanachama na kutumia rasilimali za vikundi kwa maslahi yao binafsi huku akiongeza kuwa serikali ya awamu ya tano haitavumilia vitendo vya aina hiyo na kikundi chochote kitakachoenda kinyume na taratibu za uanzishwaji wake basi kitafutiwa usajili wake.

Akimkaribisha mgeni rasmi afisa maendeleo wa kata ya Kawekamo ndugu Telesphory Balusha amesema kuwa manispaa ya Ilemela itaendelea kutoa mikopo ya kina mama, vijana na walemavu kwa haki na usawa ili wananchi wake waweze kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazowasaidia kujikwamua na umasikini.

Akihitimisha shughuli hiyo mwenyekiti wa kikundi hicho ndugu Exaud Richard ameishukuru serikali na viongozi wa kata hiyo kwa namna wanavyoshirikiana na kikundi chake katika kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo huku akiahidi kurudisha faida inayozalishwa na kikundi hicho kwa jamii kwa kusaidia  utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: