Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Professa Idris Kikula ameagiza lijengwe haraka banda la dharura pembeni ya lango kuu la ukuta wa madini ya Tanzanite, Mirerani kwa ajili madalali badala ya kwenda kuyanunulia ndani.

Kauli hiyo aliitoa juzi wakati wa ziara ya wajumbe wa tume hiyo waliotembelea eneo hilo wakifuatana na Kamishna wa Tume, Professa Abdulkarimu Mruma na mwanasheria wa tume.

Tume hiyo ilifanya ziara katika migodi hiyo kufahamu undani wa shughuli za madini zinavyofanyika, kubaini changamoto na kuzitafutia ufumbuzi ili kuimarisha na kuendeleza sekta ya madini.

Akizungumza katika eneo la Mirerani, Profesa Kikula alisema wamelazimika kutoa maagizo hayo   kuepuka upotevu zaidi wa madini hayo.

“Hatuwezi kusubiri, tumewapa maagizo wajenge haraka banda la hawa wanunuzi ili waishie pale kwenye lango kuu tukiacha tunaweza kuendelea kupoteza,” alisema Profesa Kikula na kuongeza:

“Huwezi kujua brokers wakiingia ndani na baadaye kutoka wanaweza kuficha Tanzanite kwenye nini… wanaweza kuweka hata ndani ya gurudumu la gari, pale kuna mambo mengi yanafanyika lazima tuendelee kudhibiti,” alisema.

Alisema katika ziara hiyo walibaini matofali  yaliyopangwa nje ya ukuta huo hali inayoonyesha kuna watu wanaingia au kutoka nje kwa njia isiyo rasmi.

“Tumeomba waongeze ulinzi na ukaguzi pamoja na mambo mengine tutaandika ripoti yetu na kuieleza wizara husika,” alisema Profesa Kikula na kuongeza:

“Upo upungufu tuliouona pale, eneo lile lina watu wengi   wanaoingia ndani na kila mtu ana kazi yake, pale tumekuta kuna udanganyifu kutoka kwa wanunuzi wakienda kununua ndani wanapotoka husema hawajanunua madini wakati si kweli”.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula aliyetembelea eneo hilo jana, alisema wamejipanga kuhakikisha mapendekezo na ushauri wa tume hiyo yanafanyiwa kazi.

“Kwenye lango kuu bado hatujapata vifaa kwa ajili ya uchunguzi kwa watu wanaopita mlangoni, vifaa havijafungwa na ulinzi unaofanyika ni wa kawaida.

“Sisi hata kabla ya tume tayari tulishaeleza tunahitaji CCTV camera na scana, tayari Serikali ipo kwenye maandalizi ya kuvileta   vianze kazi haraka,” alisema Chaula.

Alisema kwa sasa, wameanza kuzuia magari yote yasiyo na ulazima wa kufika kwenye migodi  yasisababishe usumbufu katika ukaguzi kwa wanaopita kwenye lango la ukuta huo.

“Kuna magari yanayobeba baruti, maji na vitu vingine muhimu, haya yanaingia kwa ukaguzi na uangalizi mkali wa kusindikizwa yakimaliza kushusha mizigo yao tunawasindikiza mpaka watoke,” alisema
Share To:

msumbanews

Post A Comment: